Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

WANANCHI TATUENI MIGOGORO KWA NJIA MBADALA, DKT. NDUMBARO

Imewekwa: 01 Feb, 2023
WANANCHI TATUENI MIGOGORO KWA NJIA MBADALA, DKT. NDUMBARO

Na William Mabusi - WKS

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amewataka wananchi kutatua migogoro na kesi kwa njia mbadala kama usuluhishi ama majadiliano badala ya kukimbilia mahakamani hali inayopekea kuingia gharama na kupoteza muda.

Dkt. Ndumbaro ameyasema hayo alipotembelea maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea kwenye viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma tarehe 26 Januari, 2023 akibainisha kuwa njia hizi zimekuwa zikileta masuluhisho ya migogoro kwa haraka na kwa gharama nafuu zaidi.

“Ujumbe wa Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka huu ni utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala  ambapo njia za maridhiano, usuluhishi, upatanishi na mashauriano zinatumika kumaliza kesi na migogoro.” Alisema Dkt. Ndumbaro.

Kuhusu kuharakisha usajili wa Wasuluhishi wa migogoro kwa njia mbadala  Dkt. Ndumbaro amesema Wizara inatumia mifumo ya TEHAMA ambapo maombi ya usajili kwa watoa huduma hupokelewa kwa njia ya mtandao bila kuwataka kufika ofisi za Wizara.

“Popote alipo mwombaji anaingia kwenye tovuti ya Wizara na kujaza fomu ya maombi, maombi yanachakatwa na usajili kukamilika endapo ombi limekidhi vigezo vyote na cheti cha usajili kutumwa kwa njia hiyo hiyo ya mtandao.” Aliongeza Waziri Ndumbaro.

Aidha sheria ya utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala imepelekea kuundwa kwa Taasisi ya Utatuzi wa Migogoro kwa Njia Mbadala Tanzania yaani Tanzania Arbitration Centre ili Wafanyabiashara, Wawekezaji na wananchi wengi kwa ujumla kupata huduma ya utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala kwa haraka.

Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Sheria kwa mwaka 2023 ni tarehe 1 Februari, 2023 ambapo Mgeni Rasmi atakuwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.