Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Wananchi watakiwa kuunga mkono jitihada za Serikali kupinga ukiukwaji wa haki za binadamu

Imewekwa: 11 Dec, 2023
Wananchi watakiwa kuunga mkono jitihada za Serikali kupinga ukiukwaji wa haki za binadamu

Na George Mwakyembe & William Mabusi – WKS Dodoma

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) ametoa wito kwa wananchi kuunga mkono jitihada za Serikali ili kuleta matokeo chanya katika kupinga vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu, rushwa na mmomonyoko wa maadili akiwataka wanachi wanapobaini vitendo hivyo kutoa tarifa kwenye vyombo vya sheria ili wahusika wachukuliwe hatua.

Waziri Mkuu ameyasema hayo alipokuwa akihutubia wakati wa kufunga maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa leo tarehe 10 Desemba, 2023 hafla iliyofanyika Viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma yakiongozwa na kauli mbiu isemayo "Zingatia maadili, utu, uhuru na haki kwa watu wote kwa maendeleo endelevu."

Mhe. Majaliwa amesema “Wananchi ninyi ni wadau wakubwa wa kutokomeza rushwa, kukomesha vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu. Ili nchi yetu isiwe na vitendo vya rushwa, isiwe na vitendi vya ukiukwaji wa haki za binadamu nyie mnapaswa kufichua matendo hayo na kupeleka taarifa kwenye vyombo husika katika kusimamia na kudhibiti matendo hayo, mwananchi usikubali kutoa rushwa popote unapotakiwa kupata huduma.”

Katika kukabiliana na dhuruma ya rushwa amesema nchi imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwa na Mkakati wa Kitaifa wa kupambana na rushwa ambao hadi sasa umetekelezwa kwa Awamu Tatu na katika hafla hiyo alizindua Mkakati wa Nne wa kupambana na rushwa ili uanze kutumika rasmi huku akiagiza elimu ya utekelezaji wa Mkakati huo iendelee kutolewa ili kuwawezesha wadau wote kuwa na uelewa wa pamoja katika kushiriki kutekeleza Mkakati huo.

Awali akitoa salaam kwenye hafla hiyo Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) amezishukuru Wizara na Taaasisi ambazo kwa wiki nzima zimeshiriki kutoa elimu juu ya haki za binadamu, rushwa, vitendo vya ukatili wa kijinsia. Aidha, Wizara hizo pia zilitoa huduma na kutatua malalamiko kutoka kwa wananchi. Amevishukuru Vyombo vya Habari kwa kurusha vipindi kwenye redio na TV na kutoa taarifa za maadhimisho hayo tangu yalipozinduliwa tarehe 3 Desemba, 2023.

Maadhimisho hayo yanaenda sambamba na maadhimisho ya miaka 75 ya Tamko la Dunia kuhusu haki za binadamu la mwaka 1948 ambapo Tanzania ni miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa iliyoridhia mikataba mbalimbali ikiwemo ya  haki za binadamu ya Kikanda na Kimataifa.