WATUMISHI MUISHI KWA UPENDO KWAKUWA MNATUMIA MUDA MREFU PAMOJA KAZINI

Watumishi wa Umma wameaswa kuishi pamoja kwa Upendo, ushirikiano na kuheshimiana kwa kila kada kwani kila mmoja ana umuhimu katika jamii na wanatumia muda mwingi pamoja wawapo kazini.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu kutoka Tume ya Haki za Binadamu Jakson Elias Nyamwihula leo Julai 1, 2025 wakati akifungua mafunzo elekezi kwa watumishi 73 wapya (walio hamia na walioajiriwa) kutoka Wizara ya Katiba na Sheria na Tume ya Haki za Binadamu.
Nyamwihula ameongeza kuwa, mafunzo hayo ni muhimu kwani ni takwa la kisheria linalowataka waajiri wote kutoa mafunzo elekezi kwa watumishi wanao ingia katika utumishi wa Umma ili waweze kuelekezwa taratibu zinazoendana na taasisi husika pamoja na kukumbushwa sheria, taratibu, kanuni na miongozo ya utendaji katika utumishi wa umma.
Amesema baada ya mafunzo haya watumishi hawa wataweza kutoa huduma bora kwa wananchi, wataweza kutunza siri kwa kutambua mipaka ya taarifa wanazo fanyia kazi, kujiepusha na vitendo vya rushwa pamoja na kufanya kazi kama timu moja.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Fatuma Kalovya, amesema mafunzo haya yametolewa ili kuimarisha utendaji kazi wa watumishi hawa na hutekelezwa kwa namna ambayo mkuu wa taasisi anaona inafaa.
“Mafunzo haya ilikuwa yafanyike mapema sana ila licha ya kuchelewa kidogo yameweza kufanyika kwa ufanisi ambapo viongozi wetu wameweza kuelekeza pia watumishi waliohamia katika Wizara na Tume ya Utumishi wa Umma waweze kupata mafunzo hayo wakijumuishwa pamoja na wale watumishi wapya”, amefafanua Kalovya.