Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Waziri Chana Afanya Kikao na Viongozi wa Taasisi ya Usuluhishi Tanzania

Imewekwa: 29 Jan, 2024
Waziri Chana Afanya Kikao na Viongozi wa Taasisi ya Usuluhishi Tanzania

Na George Mwakyembe - WKS Dodoma.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amekutana na kufanya kikao na viongozi kutoka Taasisi ya Usuluhishi wa migogoro ya Kibiashara kwa Njia Mbadala - TIArb (Tanzania Insitute of Arbitrators) na kujadili masuala mbalimbali ya namna ya kutatua migogoro kwa njia ya mapatano badala ya kwenda mahakamani.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika tarehe 29 Januari, 2024 Jijini Dodoma, Mhe. Balozi Chana amesema ni vyema taasisi hiyo ikaweka nguvu kubwa  katika kujitangaza (Branding) ili wananchi waweze kujua na kutambua umuhimu wa kutatua migogoro kwa njia ya amani. 

“Kutatua migogoro nje ya Mahakama kunajenga ushirikiano kwenye jamii zetu lakini pia kunaondoa chuki baina ya wagombanao, ni gharama nafuu na inachukua muda mfupi. Hivyo ni lazima kuwaeleza na kuwaelimisha watanzania kutumia njia hizi za utatuzi wa migogoro badala ya kukimbilia mahakamani” Alisema Waziri Chana.

Naye, Makamu wa Rais wa Taasisi hiyo Ndg. Anderickson Njunwa alieleza kuwa wao kama taasisi wamejipanga kuhakikisha wanatoa elimu kwa watanzania pamoja na semina mbalimbali za namna ya kutatua migogoro kwa njia ya upatanishi na mashauriano  ili kupunguza kesi mahakamani lakini pia kujenga upendo na  ushirikiano  katika jamii zetu.

Akiongelea mikakati mbalimbali ambayo taasisi hiyo inaendelea kuitekeleza, Bwana Njunwa alisema kwa mwaka huu tayari wameweka mkakati wa kuendesha semina na mikutano mbalimbali kwa lengo la kuwajengea uwezo wasuluhishi pamoja na watatuzi wa mogogoro.

Taasisi ya Usuluhishi Tanzania (TIArb) ilisajiliwa Desemba 1999 na Msajili wa Vyama kwa Cheti cha Usajili Namba 8833. Kazi kubwa ya TIArb ni kukuza na kuwezesha utatuzi wa migogoro ya kibiashara nchini Tanzania. Kabla ya kuanzishwa kwake, Baraza la Kitaifa la Ujenzi (NCC) lilikuwa likichukua jukumu kama hilo kwa migogoro inayohusiana na ujenzi pekee.