Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Waziri Chana Aipongeza Tume ya Kurekebisha Sheria

Imewekwa: 23 Sep, 2023
Waziri Chana Aipongeza Tume ya Kurekebisha Sheria

Na George Mwakyembe & Faraja Mhise - WKS

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amekutana na Menejimenti pamoja watumishi wa Tume ya Kurekebisha Sheria ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake zenye lengo la kuyafahamu majukumu ya Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria tangu ateuliwe kuwa Waziri wa Wizara hiyo. 

Akiongea na watumishi hao tarehe 22 Septemba, 2023 katika ofisi za Tume ya Kurekebisha Sheria zilizopo Jijini Dodoma, Mhe. Chana amewapongeza kwa kazi kubwa wanayofanya ya utafiti wa marekebisho ya Sheria pamoja na kutunga Sheria mpya zenye kuendana na wakati.

“Tume hii imekuwa ikifanya vizuri katika ukanda wa Afrika Mashariki pamoja na ukanda wa Kusini mwa Bara la Afrika na imekuwa mfano wa kuigwa, pia Tume hii imekuwa ikifanya mapitio mbalimbali ya Sheria muhimu katika nchi yetu, na  wanasheria kutoka nchi nyingine  wamekuwa wakija kujifunza hapa, nawapongeza sana,“ amesema Mhe. Chana.

Aidha, Mhe. Chana ameongeza kuwa Tanzania ni nchi yenye amani, utulivu pamoja na usalama   kwasababu ya kuzingatia Sheria na taratibu za misingi bora ambayo imewekwa. Waziri Chana aliongeza kuwa Sheria za Tanzania ni bora na ubora wake unatokana na utafiti mzuri unaofanyika kabla ya kuzitunga sheria hizo lakini pia marekebisho ya Sheria zenyewe yanayofanyika kila inapohitajika.

Pamoja na pongezi hizo pia Mhe. Chana alipokea ripoti za mapitio ya mfumo wa sheria inayohusu mdhamini na mapitio ya mfumo wa Sheria inayohusu maadili ambayo imefanyiwa utafiti na Tume ya kurekebisha Sheria na kuahidi kushirikiana na Tume katika kushughulikia mambo kadhaa ya kiutendaji yanayoikabili Tume ikiwemo upungufu wa watumishi ili kuleta mabadiliko makubwa katika maendeleo ya Tume na Wizara.

Katika kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu Dkt. Khatibu Kazungu alisema ufanyaji wa tafiti za Sheria ambazo zinakidhi mahitaji kutokana na wakati uliopo ni mkakati wa Wizara katika kuhakikisha Sheria ambazo zinatakiwa kufanyiwa marekebisho basi zinafanyiwa tafaiti ili ziweze kurekebishwa.  

Naye, Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji mstaafu January Msofe amempongeza Waziri Chana kwa kuendelea kuaminiwa na Mhe. Rais na kuteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria. Mwenyekiti huyo akagusia baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Haki Jinai likiwemo suala la maadili, vifungo vya watoto,  ulipaji wa fidia  kwa wathirika na vifungo, kuwa yote hayo  yanafanyiwa utafiti  ili kupata Sheria zilizo bora na tayari wamejipanga kuhakikisha kuwa  yote yaliyopendekezwa  na Tume ya Haki Jinai yanafanyiwa kazi  kwa manufaa ya Watanzania.