Waziri Katiba na Sheria Aipongeza Mahakama kwa Kuiheshimisha Tanzania Kimataifa
Na. Faustine Kapama-Mahakama na Sade Soka-UDSM
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Pindi Chana tarehe 15 Septemba, 2023 amemtembelea Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ofisini kwake jijini Dar es Salaam na kufanya naye mazungumzo mafupi ambapo ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuiheshimisha Tanzania kimataifa.
Mhe. Balozi Chana, ambaye aliongozana na Naibu Waziri, Mhe. Pauline Gekul na Mkurugenzi wa Huduma za Sheria kwa Umma kutoka Wizara hiyo, Bw. Abdulrahman Mshamu, amesema Tanzania ni miongoni mwa Nchi ambayo masuala ya utawala wa Sheria yanazingatiwa.
“Tunapata fursa wakati mwingine kwenda Nchi mbalimbali, ukienda huko duniani ndipo utakapojua kwamba Tanzania tupo vizuri. Niliwahi kwenda (sehemu) nikaambiwa hapa hakuna Bunge, Mahakama haieleweki, kwa kweli sisi tupo mbali. Mhimili wa Mahakama unatuheshimisha kama Taifa, tunakupongeza sana,” Waziri Chana alimwambia Jaji Mkuu.
Ameeleza dhumuni la kumtembelea ni kujitambulisha na kujifunza mambo mbalimbali yanayofanyika katika Wizara yake, kama alivyofanya kwenye taasisi zingine, ikiwemo Shule ya Sheria kwa Vitendo na kuahidi kushirikiana na Mahakama kushughulikia mambo kadhaa ya kiutendaji yanayoikabili Shule hiyo.
“Tunawaomba sana msiache kutushauri kuhusu suala hili la Shule ya Sheria kwa Vitendo, ninyi mmebobea kwenye vyuo hivi, mnaweza kushauri tuboreshe wapi, haiwezekani kwa nini watu walalamike kuwa hawafaulu kwenye masomo yao. Milango yetu ipo wazi, mkitaka maboresho ya bajeti, sheria na kanuni, haya ni majukumu yetu, sisi tutakuwa tayari muda wowote,” amesema.
Naye Naibu Waziri amemshukuru Jaji Mkuu kwa kuimarisha utendaji katika Mahakama ya Tanzania kwani picha iliyopo huko nje, hasa katika Magereza, ni nzuri kwani wafungwa na mahabusu wanaridhishwa na kasi ya usikilizaji wa mashauri yao.
“Picha iliyoko huko ni nzuri kwa kweli, tumekuwa tukitembelea Magereza tunakutana na mahabusu na wafungwa, wanawapongeza sana na wamefurahi namna wanavyo angaliwa vizuri na Mahakama, nakala zao za hukumu wanazipata kwa wakati, kesi zinasikilizwa, hivyo wanaishukuru Mahakama kwa kazi hii nzuri,” amesema.
Kadharika, amemshukuru Mhe. Prof. Juma kwa kuwawezesha kama Viongozi wa Wizara ya Katiba na Sheria kujionea miradi mbalimbali inayotekelezwa na Mahakama, hatua inayomsaidia kujibu kwa ufasaha maswali anayokutana nayo Bungeni.
“Naupongeza Uongozi wa Mahakama kwa kushirikiana nami na kuwa tayari kunisaidia katika hatua mbalimbali, ikiwemo kujibu maswali ninayoyapata Bungeni, hasa suala hili la miradi inayoendelea kutekelezwa, ikiwemo ujenzi wa Mahakama za Mwanzo 60,” amesema.
Akizungumza na wageni wake, Jaji Mkuu alimpongeza Waziri Chana kwa kuaminiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwa kiungo muhimu kati ya Serikali na Mhimili wa Mahakama.
Amemkaribisha kuitembelea Mahakama mara kwa mara ili kujifunza shughuli mbalimbali zinazofanywa na Mhimili huo.
“Kuna maeneo ambayo yanasukuma maboresho ya Mahakama. Kitengo cha Maboresho ni injini, haya maboresho yanayoendelea kuna watu ambao wapo masaa 24 wakiangalia kitu gani kipo wapo, majengo yakoje, TEHAMA ipo vipi, tuna Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia, ni Dunia nyingine kabisa. Hivyo, haya ni maeneo ambayo ni muhimu sana ukiyaelewa,” Mhe. Prof. Juma amemweleza Waziri Chana.
Jaji Mkuu amemshukuru Waziri kwa kuendelea kuiongelea Mahakama katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Bungeni kwa kuzingatia mambo mengi yanayofanyika hayafahamiki kwa umma kwa kiwango cha kuridhisha. “Ukisoma kwenye magazeti kuhusu Mahakama au Wizara utashangaa kama hao wanaoandika wanaishi Tanzania. Nadhani tunajukumu la kuuhabarisha umma,” amesema.
Kuhusu Shule ya Sheria kwa Vitendo, Mhe. Prof. Juma amekubaliana na Waziri kuwa ni eneo ambalo wanahitaji kulifanyia kazi kwa kushirikisha Wizara na Mahakama kwa pamoja ili kutafuta namna ya kutatua changamoto zinazoibuliwa, hasa katika kuimarisha elimu kwa vitendo kwa wanafunzi.
Kwa upande wake, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani amesema Mahakama imekuwa ikishirikiana na Shule ya Sheria kwa Vitendo katika kufanya maboresho na kuanzia Januari mwakani wanatarajia kutakuwa na mitaala mipya, hatua ambayo itasaidia kubadilisha hali ya Shule hiyo.
“Toka mwanzo ilionekana elimu iliyokuwa inatolewa ilikuwa nadhalia zaidi, ile practical aspect ambayo inatarajiwa wanafunzi wanapokuwa katika hatua za mwisho kabisa za kuhitimu taaluma yao waipate ilikuwa changamoto. Kwa hiyo, Mahakama imeshiriki kwenye maboresho makubwa,” amebainisha.
Jaji Kiongozi ameshukuru mtazamo wa Wizara kuhusu Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwani ni rahisi zaidi baada ya kufanya kazi kwa muda mrefu kama kitakuwa moja kwa moja chini ya Mahakama, hatua ambayo itaimarisha zaidi utendaji wake.
Akizunguza katika tukio hilo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel alimfahamisha Waziri maeneo manne ambayo wanaweza kuyatembelea, Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia, Kitengo cha Maboresho cha Mahakama ya Tanzania, Kituo cha Huduma kwa Mteja Kinondoni, Tume ya Utumishi wa Mahakama na Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Biashara.