WAZIRI LUKUVI AMTAKA MKANDARASI KUKAMILISHA UJENZI WA JENGO LA OFISI YA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. William Vangimembe Lukuvi amemtaka mkandarasi SUMA JKT anaye tekeleza mradi wa ujenzi wa jengo la ofisi ya Wizara ya Katiba na Sheria kukamilisha ujenzi huo kwani tayari amekwisha lipwa fedha zote na muda wa utekelezaji wa mkataba umepita.
Waziri Lukuvi ametoa agizo hilo leo Julai 23, 2025 mara baada ya kutembelea na kufanya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo lililopo mji wa Serikali Mtumba Jijijini Dodoma na kuongeza kuwa nia ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ya Kutaka Serikali na Wizara ziwe sehemu moja iheshimiwe.
“Mhe. Rais aliamua kujenga majengo ya kudumu ya Mji wa Serikali ili wizara zote zije hapa, ninyi SUMA JKT mkaheshimika kupata mradi huu, haifurahishi kuona mnaongezewa muda, ilitakiwa mkamilishe ujenzi mwezi Mei 2025 na mmeshalipwa fedha zote, hivyo basi nawataka mkamilishe mwezi Agosti kama mlivyoahidi”, amesisitiza.
Waziri Lukuvi ameongeza kuwa Mwezi Agosti atatembelea tena ili kukagua endapo mkandarasi atakuwa amekamilisha ujenzi huo kama alivyo omba kuongezewa muda huku akimtaka Katibu Mkuu ofisi ya Waziri Mkuu kuendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa mradi huo.
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Dkt Franklin Jasson Rwezimula amesema mkandarasi alipewa mradi huo Agosti 2025 ambapo alitakiwa kukamilisha ujenzi Februari 2022 ambapo muda wa utekelezaji umeongezwa hadi Agosti 2025.
Dkt Rwezimula ameongeza kuwa hadi sasa ujenzi umekamilika kwa asilimia 90 huku akieleza kuwa baadhi ya kazi zilizobakia ni pamoja na kazi za umeme, kupaka rangi ndani ya jengo, handles za milango na kuweka jenereta.
Aidha upande mmoja wa jengo hilo umekamilika na baadhi ya vyumba katika jengo hilo vinatarajiwa kuanza kutumika mapema wiki ijayo mara baada ya kukamilika kwa shughuli ya usafi.