WAZIRI NDUMBARO AAGIZA ANDIKO LA HISTORIA YA TANZANIA NA MABORESHO YA SEKTA YA HAKI JINAI

Waziri wa Katiba na Sheria Dkt Damas Ndumbaro amewaagiza watalaam wa Wizara hiyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuanza mchakato wa kuandaa andiko litakalo onyesha historia ya Tanzania na maboresho yaliyo fanyika katika sekta ya haki jinai kwani hadi sasa yamesha fanyika maboresho mengi.
Waziri Dkt Ndumbaro ambaye ni Mwenyekiti wa kikao cha Jukwaa la Haki Jinai kwa Kamati ya Mawaziri, ametoa agizo hilo jana Juni 25, 2025 katika ukumbi wa Bunge wa Frank Mfundo wakati akiendesha kikao hicho kilichowahusisha, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais UTUMISHI, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Waziri Dkt Ndumbaro amesema lengo la kikao hicho ni kujadiliana masuala mbalimbali yanayohusu mfumo wa Haki Jinai Nchini ikiwa ni utekelezaji wa moja ya mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai ambayo iliundwa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan.
Naye Naibu Waziri Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mwanaidi Ali Khamis amesema Wizara yake kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza Nchini inaendelea na mchakato wa kujenga shule za maadilisho kwa ajili ya watoto walio chini ya miaka 18 waliokinzana na sheria na kupata adhabu za vifungo.
Naibu Waziri Mwanaidi ameongeza kuwa kwa upande wa kanda ya Ziwa shule za maadilisho kwa watoto wa kike waliokinzana na sheria na kupata adhabu za vifungo zinajengwa na Mkoa wa Mwanza ni mojawapo ya mkoa ambapo ujenzi unaendelea.
Kwa Upande wake Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Innocent Bashungwa ameeleza kuwa Wizara yake kupitia Jeshi la Magereza inaendelea na mchakato wa kutoa mafunzo ya ufundi stadi ikiwa ni mbinu mojawapo ya kuwafanyia urekebu wafungwa ambapo hadi sasa jumla ya wafungwa 201 wamehitimu mafunzo hayo.
Taasisi nyingine zilizo shiriki mkutano huo ni pamoja na Jeshi la Magereza, Jeshi la Uhamiaji, PCCB, DCI, DCE, JoT na NPS.