Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Wizara Kuendelea Kuboresha Sheria – Dkt. Chana

Imewekwa: 02 Feb, 2024
Wizara Kuendelea Kuboresha Sheria – Dkt. Chana

Na William Mabusi – WKS Dodoma

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria itaendelea kuzifanyia utafiti na kuboersha sheria zote zinazotakiwa kufanyiwa mabadiliko.

Dkt. Chana amesema hayo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Tabora Mjini Mhe. Emmanuel Adamson Mwakasaka, aliyetaka kujua lini Serikali italeta Bungeni Sheria mahsusi kwa ajili ya kuwalinda wananchi dhidi ya Ukatili wa Kijinsia.

Amesema “tunazo Sheria zinazowalinda wananchi dhidi ya ukatili wa kijinsia ambazo ni Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16, Sheria ya Ndoa Sura ya 29, Sheria ya Mtoto Sura ya 13, Sheria ya Makosa ya Mtandao Sura ya 443 na Sheria ya Kuzuia Usafirishaji Haramu wa Binadamu Sura ya 432. Kwa pamoja Sheria hizo zina vifungu vinavyozuia makosa ya ukatili wa kijinsia, zote kwa pamoja zina vifungu vinavyoshugulika na makosa ya ukatili wa kijinsia. Hata hivyo, Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara nyingine za kisekta ikiwemo Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Makundi Maalum, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania na wadau mbalimbali tunaendelea na uchambuzi ili kubaini iwapo ipo haja ya kuwa na sheria mahsusi ya ukatili wa kijinsia au tuboreshe sheria zilizopo. Baada ya kukamilika kwa uchambuzi huo Serikali itachukua hatua stahiki.”

Aidha, Dkt. Chana amewataka Wananchi kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia Vituo vya Polisi bila hofu ili sheria ichukue mkondo wake huku akisisitiza kuwa watoa taarifa na mashahidi nao wanalindwa na sheria ya kuwalinda Watoa taarifa na Mashahidi ya mwaka 2015.

Akijibu swali la Mbunge wa Ukerewe Mhe. Joseph Michael Mkundi aliyetaka kujua lini Serikali itakarabati na kujenga Mahakama mpya ya Wilaya ya Ukerewe. Dkt. Chana amesema Serikali kupitia Mahakama ina mpango wa kujenga na kuboresha majengo ya Mahakama katika ngazi mbalimbali, katika utekelezaji wa mpango huo Serikali imepanga kujenga Mahakama ya Wilaya ya Ukerewe katika mwaka wa fedha 2024/25.