Wizara kuimarisha mfumo wa mwanamke kupata haki kwa wakati
Na William Mabusi – WKS
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amezindua Jukwaa la Kitaifa la Haki Mwanamke lenye lengo la kurahisisha upatikanaji haki kwa mwanamke na kwa wakati, kuimarisha mifumo ya upatikanaji haki kwa mwanamke katika kesi za jinai na pia katika kesi za madai.
Uzinduzi wa jukwaa hilo umefanyika tarehe 06 Juni, 2023 jijini Dodoma na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa haki hapa nchini, wakiwemo baadhi ya Waheshimiwa Wabunge, Wadau wa Maendeleo, Asasi za Kiraia, Idara na Taasisi za Serikali.
“Wizara ya Katiba na Sheria itaendelea kushirikiana na wadau wote katika kuhakikisha tunapaza sauti kuhusiana na mambo mbalimbali zikiwemo haki za binadamu, na leo tunaongelea haki ya mwanamke.” Alisema Dkt. Ndumbaro.
Usimamizi wa haki nchini ni jukumu la Wizara ya Katiba na Sheria kwa mujibu wa Haki Idhini iliyotolewa na Mhe. Rais. Kutokana na idhini hiyo Wizara iliunda Jukwaa la Haki ya Mtoto ambalo linatekeleza jukumu lake vizuri katika kulinda haki za mtoto na sasa Wizara imeanzisha Jukwaa la Haki Mwanamke ambapo walengwa wakubwa ni wanawake katika ngazi zote kuanzia ngaza ya kitaifa hadi mwanamke wa kijijini.
Jukwaa hilo litakuwa la kipekee kuwezesha upatikanaji wa taarifa na ushahidi katika masuala yanayoathiri wanawake na changamoto zinazowakabili. Aidha, Jukwaa litabainisha maeneo ya kimkakati ambayo yatatengenezewa mikakati na kuweza kutekelezwa ili kusaidia mwanamke kuweza kupata haki, kuimarisha mfumo wa upatikanaji wa takwimu ambazo zitawezesha Serikali kuweza kupanga mikakati ya namna ya ufikiwaji wa haki kwa mwanamke.
Akitoa salaam katika hafla hiyo Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Bi. Pauline Gekul (Mb) ambaye amepewa jukumu la kulea Jukwaa hilo amesema Jukwaa Haki Mwanamke si tu litawafikia wanawake bali litakwenda kwa kasi, na litawafikia wanawake kwenye Kata zote nchini kuwapa elimu kuhusu masuala ya upatikanaji wa haki ili wakipata changamoto wafahamu sehemu sahihi za kwenda kupata haki zao.
Naye Bi. Mary Makondo Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria amesema katika kuimarisha upatikanaji wa haki kwa makundi maalumu, Wizara imekuwa ikitekeleza Mpango Kazi wa Kitaifa wa kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Katika utekelezaji wa mpango huo Wizara imeweza kuimarisha mifumo ya sheria ikiwemo kutungwa kwa sheria ya Msaada wa kisheria na kupitia sheria hiyo wanawake wamekuwa wanafaidika kisheria kwenye maeneo yao.