Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

WIZARA  NA JESHI LA MAGEREZA KUSHIRIKIANA UTOAJI HUDUMA ZA MSAADA WA KISHERIA MAGEREZANI

Imewekwa: 05 Jun, 2026
WIZARA  NA JESHI LA MAGEREZA KUSHIRIKIANA UTOAJI HUDUMA ZA MSAADA WA KISHERIA MAGEREZANI

Majadiliano ya kuimarisha ushirikiano katika utoaji wa huduma za msaada wa kisheria magerezani yamefanyika kati ya Wizara ya Katiba na Sheria na Jeshi la Magereza nchini, yakilenga kuhakikisha haki inapatikana kwa wafungwa na mahabusu kwa mujibu wa sheria pamoja na kuimarisha mifumo ya utoaji huduma katika taasisi hizo.

Akizungumza wakati wa kikao hicho kilichofanyika Juni 03, 2026, Mtumba Jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria amesema ushirikiano kati ya taasisi hizo mbili ni hatua muhimu katika kuendeleza dhamira ya Serikali ya kuhakikisha haki inapatikana kwa wote, ikiwemo watu walioko magerezani na mahabusu ambao wanahitaji msaada wa kisheria ili kutambua na kutetea haki zao kwa mujibu wa sheria za nchi.

Dkt, Jingu amesema kupitia ushirikiano huo, Wizara na Jeshi la Magereza zitaendelea kushirikiana katika kuimarisha huduma za msaada wa kisheria kwa wafungwa na mahabusu, jambo litakalosaidia kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza katika upatikanaji wa haki na kuongeza uelewa wa sheria kwa wahusika.

Aidha Dkt. Jingu ametaja maeneo muhimu ya ushirikiano huo ni kuwajengea uwezo wataalamu wanaotoa huduma za msaada wa kisheria magerezani kupitia mafunzo na mbinu mbalimbali zitakazowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi, kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa haki kwa kutumia mbinu za kisasa zitakazorahisisha utoaji wa huduma za kisheria kwa makundi yote yanayohitaji huduma, matumizi ya TEHAMA kama nyenzo muhimu katika kuboresha utoaji wa huduma za kisheria, na kuimarisha mifumo ya kidijitali inayowezesha upatikanaji wa taarifa kwa wakati na kuongeza ufanisi katika utendaji wa kazi.

Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Magereza, Jeremiah Katundu, ameishukuru Wizara ya Katiba na Sheria kwa ushirikiano mkubwa unaoendelea kutolewa kwa Jeshi la Magereza, hususan katika kuwajengea uwezo maafisa wa magereza kupitia mafunzo na programu mbalimbali zinazolenga kuimarisha utoaji wa huduma za msaada wa kisheria.

Kamishina Katundu amesema msaada wa kisheria unaotolewa kwa wafungwa na mahabusu umekuwa na mchango mkubwa katika kuwawezesha kufahamu haki zao na taratibu za kisheria, huku akieleza kuwa juhudi hizo zimeongeza ufanisi katika utoaji wa haki ndani ya magereza. Pia ameishukuru Wizara kwa kukabidhiwa vifaa vya TEHAMA vilivyosaidia kuboresha mawasiliano na utekelezaji wa majukumu ya kila siku.

Kamishina ameahidi kuwa Jeshi la Magereza litaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Wizara ya Katiba na Sheria katika kutekeleza mipango mbalimbali inayolenga kuimarisha huduma za msaada wa kisheria na kuhakikisha haki inatendeka kwa wote bila hofu wala wasiwasi, sambamba na kuendeleza misingi ya utawala bora na haki nchini.