Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

WIZARA YA KATIBA NA SHERIA YAPATA TUZO YA MSHINDI KWANZA SABASABA MAKUNDI YA WIZARA

Imewekwa: 08 Jul, 2025
WIZARA YA KATIBA NA SHERIA YAPATA TUZO YA MSHINDI KWANZA SABASABA MAKUNDI YA WIZARA

Wizara ya Katiba na Sheria imepokea tuzo ya Mshindi wa Kwanza katika kundi la Wizara zote zilizoshiriki maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba 2025).

Tuzo hiyo imetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi wakati wa uzinduzi rasmi wa maonesho hayo yaliyojumuisha wananchi, taasisi na mamlaka mbalimbali pamoja na wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi.

Akipokea tuzo hiyo kwa niaba ya Wizara Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Dkt Franklin Rwezimula amewapongeza watumishi wote wa Wizara hiyo kwa juhudi zao kubwa kwa kuhudumia wananchi kwa weledi na ufanisi.

“Tuzo hii ni matokeo ya kujitoa kwa watumishi wetu ambao wamejituma kwa bidii kutoa elimu sahihi ya Katiba, Haki za Binadamu, uangalizi wa Utajiri wa asili na Maliasilia za Nchi pamoja na kutoa msaada wa Kisheria bure kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia”, ameeleza.

Akizungumza kwa niaba ya watumishi wa Wizara, Mkurugenzi Msaidizi, Sehemu ya Kutoa Taarifa za Haki za Binadamu Bi. Beatrice Mpembo amesema tuzo hiyo imewapa mori wa kujituma zaidi kuwahudumia wananchi.

“Tuzo hii imetupa motisha sana, tutaendelea kuwahudumia wananchi kwa bidii zaidi na tunapenda kutoa shukrani za dhati kwa wadau wote na taasisi zilizo chini ya Wizara kwa ushirikiano lakini zaidi tunaushukuru uongozi wa Wizara ukiongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria kwa maono yake na pamoja na maelekezo ya viongozi wenzake Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu wamewezesha tumefanikisha kupata tuzo hii”, ameongeza.