MAAFISA WA SERIKALI WAJENGEWA UWEZO KUHUSU MIKATABA NA SHERIA ZA KIMATAIFA
Kituo cha Ufanisi wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (African Court Coalition – ACC) kwa kushirikiana na wataalam kutoka Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu na Chama cha Wanasheria wa Afrika Mashariki (EALS) wameendesha kikao cha kuwajengea uwezo maafisa mbalimbali wa Serikali. Mafunzo hayo yamejikita katika majukumu ya Mahakama ya Afrika, sheria na mikataba ya kimataifa na kikanda.
Akifungua mafunzo hayo, Mratibu wa ACC, Sophia Ebby, alisema warsha hiyo imelenga kuimarisha uelewa wa pamoja kuhusu Mahakama ya Afrika na wajibu wa wadau mbalimbali.
"Tunatarajia kuwa majadiliano yatakayofanyika yataimarisha ushirikiano katika kuendeleza haki, utawala wa sheria na ulinzi wa haki za binadamu," alisema Bi. Ebby.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Haki za Binadamu Wizara ya Katiba na Sheria, Bi. Nkasori Sarakikya, alisema mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuimarisha upatikanaji haki kwa kuwajengea uwezo maafisa husika kwenye mnyororo wa haki.
Aliwahimiza washiriki kushiriki kikamilifu, akisisitiza kuwa Serikali inategemea utaalamu wao katika kutekeleza wajibu wake wa kukuza na kulinda haki za binadamu.