Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

DCI, CP. KINGAI ATOA WITO ELIMU YA MAKOSA YENYE DHAMANA NA YASIYO NA DHAMANA

Imewekwa: 04 Jul, 2026
DCI, CP. KINGAI ATOA WITO ELIMU YA MAKOSA YENYE DHAMANA NA YASIYO NA DHAMANA

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), CP Ramadhani Kingai, ametoa wito kwa Wizara ya Katiba na Sheria kuendelea kuimarisha utoaji wa elimu kwa jamii hususan elimu ya makosa yenye dhamana na yasiyo na dhamana.

CP. Kingai ametoa wito huo leo 4 Julai, 2026 alipotembelea banda la Wizara ya Katiba na Sheria wakati wa Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimuj Nyerere (Sabasaba), jijini Dar es Salaam, ambapo pia amepata fursa ya kujionea namna wizara inavyowahudumia wananchi kupitia elimu ya kisheria, ushauri na utatuzi wa masuala mbalimbali ya kisheria.

Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, CP Kingai aliipongeza Wizara ya Katiba na Sheria kwa jitihada zake za kupeleka huduma karibu na wananchi kupitia maonesho hayo na kusema utoaji wa elimu ya kisheria ni hatua muhimu inayosaidia kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki, wajibu na taratibu mbalimbali za kisheria nchini.

“Kuna sintofahamu kubwa sana miongoni mwa watanzania kuhusu tofauti ya makosa yenye dhamana na yale yasiyo na dhamana, jambo ambalo wakati mwingine husababisha malalamiko na tafsiri zisizo sahihi kuhusu hatua zinazochukuliwa na vyombo vya dola” alisema CP Kingai.

‘’Niwaombe Wizara ya Katiba na Sheria, kutoa elimu sahihi ya kisheria kuhusiana na aina hizi za makosa ili kuwasaidia wananchi kuelewa taratibu za uchunguzi na na uendeshaji wa mashauri ya jinai” alisisitiza CP. Kingai.
 
CP. Kingai alisema kuwa elimu hii itapunguza upotoshaji wa taarifa na kuongeza imani ya wananchi kwa taasisi zinazotekeleza sheria, sambamba na kuongeza ushirikiano kati ya vyombo vya usalama na taasisi za sheria katika kujenga jamii inayoheshimu sheria na haki.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi, Sehemu ya Usuluhishi kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Felix Chakila amesema kuwa wizara itaendelea kutumia Maonesho haya kama jukwaa la kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa kutoa elimu, ushauri na huduma mbalimbali za kisheria.