Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Dkt. Chana Azindua Kitabu “The Fatimids”

Imewekwa: 25 Oct, 2023
Dkt. Chana Azindua Kitabu “The Fatimids”

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amezindua Kitabu cha Historia ya Utawala wa Kiislamu wa Fatimid ‘’THE FATIMIDS’’ huku akimpongeza mwandishi wa kitabu hicho mwanamama Dkt. Shainool Jiwa kutoka Taasisi ya Aga Khan na kuwahimiza mabinti walioko mashuleni na vyuoni kuiga mfano.

Kitabu hicho kinachoelezea utawala wa Kiislamu unaosemekana kutawala zaidi ya miaka 250 katika mwambao wa bahari ya Atlantiki ya Afrika Kaskazini na kusini mwa bahari ya Mediterranean na pande zote za bahari ya Shamu, kimezinduliwa tarehe 25 Oktoba, 2023 Jijini Dar es Salaam.

"Nampongeza sana Dkt. Shainool Jiwa kwa utafiti wake ambao naomba ulete chachu kwa mabinti zetu ambao wako shuleni na vyuoni kuona kwamba Wanawake wanaweza kutoa mchango mkubwa kwa jamii mfano ni hili jambo kubwa la utafiti." Alisema Balozi Dkt. Chana.

Vile vile Dkt. Chana amewahimiza Wasomi mbalimbali hapa nchini kujikita katika utafiti ili kuibua historia na maisha ya vizazi vilivyopita pamoja na kuendeleza urithi wa utamaduni uliopo katika nchi yetu hasa kwa kipindi hiki ambacho Teknolojia ya Habari na Mawasiliano iko juu hivyo wananchi wanaweza kufuatilia na kuelewa kwa urahisi tafiti hizo.

Kupitia Hotuba yake kwa niaba ya Serikali Mhe. Chana ameishukuru Taasisi ya Aga Khan kwa kusaidia jamii ya watanzania katika sekta ya afya, elimu na huduma nyinginezo za kijamii katika Mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Hafla hiyo imeandaliwa na Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN) Tanzania kwa kushirikiana na Taasisi ya Taaluma ya Ismaili (Institute of Ismail Studies) ambapo Dkt. Shainool Jiwa chini ya Taasisi ya IIS London amewasilisha juzuu mbili ya kazi bora ya historia ya ukoo wa Fatimid uliotawala kuanzia miaka ya 909 – 1171 CE kama himaya ya Kiislam zilizokuwa na ushawishi mkubwa na utajiri katika ulimwengu wa Kiislam katika Zama za Kati.