HUDUMA ZA MSAADA WA KISHERIA KUWA ENDELEVU-NAIBU WAZIRI SAGINI

Naibu Waziri Wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini amesema Wizara hiyo inawahakikishia wananchi kuwa huduma za msaada wa Kisheria zitakuwa endelevu kwani uzoefu uliopatikana wakati wa Utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia umeonesha huduma hiyo ni hitaji kubwa kwa wananchi.
Mhe. Sagini ameyasema hayo leo Julai 8, 2025 katika maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba 2025) mara baada ya kutembelea banda la kutolea huduma la Wizara na mabanda ya Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo.
“Baada ya uzoefu wa miaka minne tumeridhika kuwa huduma ya Msaada wa kisheria inahitajika na ndio maana Wizara ya Katiba na Sheria inalifanya jambo hili kuwa endelevu kwa kuwapeleka maafisa ngazi ya halmashauri ili wawasaidie wananchi, Pia tunashirikiana na wadau wengine kama Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kutoa huduma za Msaada wa kisheria pamoja na maafisa Ardhi wa Mikoa kuwaeleimisha wananchi juu ya sheria ya ardhi ili kupunguza migogoro”, amesema Mhe Sagini.
Ameongeza kwa kuipongeza Mahakama Kuu kwa kuweka umuhimu katika utatuzi wa Migogoro kwa njia mbadala, pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa Kuanzisha kampeni hiyo, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuidhinisha bajeti, Wizara ya Fedha kwa kuzitoa fedha hizo, Waziri wa Katiba na Sheria kwa kuzisimamia pamoja na Katibu Mkuu kwa kuhakikisha fedha hizo zinatumika ipasavyo.
Aidha Naibu Waziri Jumanne Sagini amewapongeza watumishi wa Wizara hiyo kwa kupata tuzo ya mshindi wa kwanza upande wa Wizara zilizoshiriki kwani wameshatahili kutokana na namna wanavyohudumia wananchi vizuri na ubora wa banda hilo.
“Nimefika na kushuhudia kuwa tunastahili watu wa Katiba na Sheria kupata tuzo kwa mapokezi nayoyaona, elimu watu wanayopewa na nimezungumza na watu kadhaa waliohudumiwa kila mmoja anaridhishwa na huduma zinazotolewa na wataalamu kwakweli nawapongeza sana pia nampongeza Waziri wa Katiba na Sheria pamoja na Katibu Mkuu kwa kuleta idara zote hapa ambazo hutoa elimu za masuala mbalimbali hivyo wana Dar Es Salaama na wote wanaofika Sabasaba nawasihi msikose kupita katika banda hili”, amesisitiza Mhe. Sagini.