Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Majaliwa: Mawakili wa Serikali mna dhamana kubwa kuitetea Serikali

Imewekwa: 06 Jun, 2023
Majaliwa: Mawakili wa Serikali mna dhamana kubwa kuitetea Serikali

Na William Mabusi – WKS

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) amewataka Mawakili wa Serikali kufanya kazi kwa uzalendo na kuwa wabunifu katika kuitetea na kuishauri Serikali ipasavyo kuhusu mashauri inayokabiliana nayo ili kuiletea nchi maendeleo.

Mhe. Majaliwa ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya miaka mitano tangu kuanzishwa kwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, tarehe 05 Juni, 2023 Jijini Dodoma.

“Mawakili wa Serikali mmepewa dhamana ya kuitetea Serikali katika uendeshaji wa mashauri ya madai na usuluhishi hivyo ongezeni bidii, juhudi na weledi katika utendaji kazi wenu, kufanya kazi kwa uzalendo na kuwa wabunifu katika kuishauri Serikali ipasavyo kuhusu mashauri yaliyopo kwani maendeleo ya nchi yetu yanatokana na sisi wenyewe.”

Mhe. Majaliwa amepongeza Wizara ya Katiba na Taasisi zake kwa kusimamia vema haki na utoaji wa haki sambamba na uelimishaji wananchi kutambua haki na wajibu wao hususan katika kipindi hiki cha miaka mitatu cha utekelezaji wa Mama Samia Legal Aid Campaign ambayo inatekelezwa nchini kote na sasa imeshatekelezwa katika mikoa ya Dodoma na Manyara.

Mhe. Waziri Mkuu akiongelea kuhusu kauli mbiu katika maadhimisho hayo ambayo inasema ‘Miaka mitano ya ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali; tulipotoka, tulipo na tunapoelekea’ amesema “pasipo tathmini ni vigumu kufahamu mwenendo wa utekelezaji wa mipango yenu. Tathimini hubaini changamoto ambazo zikifanyiwa kazi hupelekea kutimiza malengo katika Taasisi.”

Akiwasilisha salaam za Mhe. Rais, Makamu wa Rais na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Waziri Mkuu amesema, “Viongozi wetu watatu Wakuu katika nchi wana matumaini makubwa na sekta ya sheria kwamba itaendelea kutoa msaada wa sheria kwa watanzania ili wale wote wenye matatizo waweze kuyatatua katika njia rahisi.”

Akimkaribisha Mgeni Rasmi, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amemshukuru Mhe. Rais kwa kuunga mkono ofisi zote za sekta ya haki.

Dkt. Ndumbaro amesema, “nachukua nafasi hii kumshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ambayo anaunga mkono sekta ya sheria hususan ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa kuongeza bajeti yake kuhakikisha kuwa kazi inaendelea.”

Akiyataja baadhi ya mafanikio ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ndumbaro amesema “ndani ya kipindi cha miaka mitano ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wamemaliza mashauri mengi kwa njia ya usuluhishi na kwa njia ya amani na hivyo kuokoa si tu gharama kwa Serikali katika kuendesha kesi hizo lakini pia fedha ambazo Serikali ingelipa endapo ingeshindwa kesi hizo. Kwa mwaka wa fedha 2022/23 ambao unaishia Juni mwaka huu Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imewezesha Serikali kuokoa kiasi cha shilingi tilioni saba nukta tatu kutokana na mashauri iliyofanya.

Akitaja maandalizi ya ndani ya mchakato wa Katiba Mpya yanayoendelea Wizarani amesema tarehe 28 na 29 Juni 2023 jijini Dodoma utafanyika mkutano maalum utakaowajumuisha Mawaziri wa Sheria wote ambao wamestaafu, Wanasheria Wakuu wa Serikali waliostaafu ili washauriane na Wizara kuhusu mchakato wa Katiba.

Naye Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniface Luhende akitoa salaam katika maadhimisho hayo amesema maadhimisho hayo yanaenda sambamba na kufanya tathmini ya malengo yaliyokusudiwa katika utendaji kazi wa miaka mitano tangu Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ilipoanzishwa tarehe 13 Februari, 2018. Aidha, maadhimisho hayo ni fursa ya kujipanga kuboresha utekelezaji wa majukumu ya ofisi yake ya kuendesha na kusimamia mashauri ya jinai na madai kwa niaba ya Serikali.