MAWAKILI WA SERIKALI, MAAFISA SHERIA KUTOA HUDUMA ZA MSAADA WA KISHERIA ILI KUONGEZA WIGO WA UPATIKANAJI HUDUMA
Wizara ya Katiba na Sheria imeandaa Mpango utakaowawezesha Mawakili wa Serikali na Maafisa Sheria ambao ni Mawakili wa Kujitegemea au wana sifa za kuwa Mawakili wa Kujitegemea kuruhusiwa kutoa huduma za msaada wa kisheria hususani uwakilishi kwa mashauri ambayo hayana mgongano wa kimaslahi na mwajiri.
Akifungua rasmi mafunzo ya Mawakili wa Serikali na Maafisa Sheria leo 28 Januari, 2026 jijini Arusha, Mkuu wa Mkoa wa Arusha CPA. Amos Makalla akimuwakilisha Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera amesema kuwa Mpango huu utawawezesha Mawakili na Maafisa Sheria kutoa huduma za msaada wa kisheria kwa jamii ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma, kuweka uendelevu wa huduma na kuimarisha ufanisi na utendaji katika kazi za sheria.
Mh. Makalla amesema kuwa ni wajibu wa Mawakili wa Serikali kuhakikisha wanaongeza uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya haki na wajibu wao kwa lengo la kuendelea kujenga Taifa lenye amani na maendeleo.
“Uhitaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa jamii ni mkubwa sana na wananchi bado hawana uelewa na masuala ya sheria, wajibu na haki zao. Ni wajibu wetu sisi Mawakili wa Serikali kuhakikisha tunaongeza uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya haki na wajibu wao kwa lengo la kuendelea kujenga Taifa lenye amani na maendeleo” alisema Mhe. Makalla.
“Nchi yetu bado ina idadi kubwa ya wananchi ambao wanahitaji msaada wa kisheria lakini hawajui wapi waende au namna ya kuupata, ni jukumu letu sote kuhakikisha tunaondoa vizuizi hivyo kwa kujitoa kwa moyo katika kutoa huduma za ProBono kama sehemu ya mchango wetu kwa jamii” aliongeza.
Aidha Mh. Makalla amewasisitiza Mawakili na Maafisa Sheria kuwa na uadilifu katika kushughulikia migogoro ya wananchi na kuhakikisha migogoro yote inashughulikiwa mpaka hatua ya mwisho na kutoa taarifa za mara kwa mara kuhusu namna migogoro hiyo ilivyoshughulikiwa.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa Mawakili wa Serikali na taasisi zote zinazotoa huduma za msaada wa kisheria ili kuhakikisha huduma hizi zinawafikia Watanzania wote kwa usawa, haki na ufanisi.