Waziri wa Katiba na Sheria nchini Tanzania Dkt. Damas Ndumbaro amesema Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia imewafikia jumla ya wananchi 2,698, 908, kati yao wanaume wakiwa ni 1, 347,325 na wanawake wakiwa 1, 351, 583 katika Mikoa 25 ya Tanzania bara.
Aidha Kampeni hiyo pia kulingana na Waziri Ndumbaro, imetekelezwa kwenye Halmashauri 179, Kata 1907, Vijiji na Mitaa 5702 vilifikiwa na kampeni hiyo huku pia migogoro 24, 691 iliyodumu kwa muda mrefu, mingine kwa zaidi ya miaka kumi, ikipokelewa na kutatuliwa, suala ambalo limewezesha amani, utulivu na utengamano miongoni mwa wanajamii.
"Migogoro hii ni migogoro ya ardhi, ndoa za utotoni, matunzo ya watoto, ndoa, jinai, ukatili wa kijinsia na migogoro 5704 ilitatuliwa na kuhitimishwa kwa njia mbadala kati ya migogoro 23, 399 ya muda mrefu iliyopokelewa." Amesema Waziri Ndumbaro.
Wakati wa uwasilishaji wa Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka 2025/26 leo Jumatano Aprili 30, 2025, Bungeni Dodoma, Waziri Ndumbaro pia ameeleza kuwa katika kuhakikisha kuwa msaada wa kisheria unakuwa endelevu kwa wananchi, Serikali pia imeanzisha madawati ya msaada wa kisheria kwenye mamlaka 184 za serikali za mitaa Tanzania bara, lengo likiwa ni kusogeza huduma na kukuza uendelevu wa msaada huo wa kisheria.