Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Serikali Kuendelea Kuimarisha Majengo ya Mahakama

Imewekwa: 02 Apr, 2024
Serikali Kuendelea Kuimarisha Majengo ya Mahakama

Na William Mabusi – WKS Dodoma

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema Serikali inaendelea kuimarisha majengo ya Mahakama katika ngazi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujenga majengo mapya na kukarabati majengo chakavu.

Dkt. Chana amesema hayo wakati akijibu maswali Bungeni leo tarehe 02 Aprili, 2024 Jijini Dodoma.

”Serikali kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania imeendelea kuimarisha majengo ya Mahakama katika ngazi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kujenga majengo mapya na kukarabati majengo chakavu kwa awamu kwa kuzingatia uwezo wa kibajeti.” Amesema Dkt. Chana akijibu swali la  Mhe. Francis Isack Mtinga Mbunge wa Wilaya ya Mkalama aliyetaka kujua ujenzi wa Mahakama kwenye Wilaya hiyo utaanza lini.

Mhe. Waziri amesema Wilaya ya Mkalama ambayo ni moja ya Wilaya nne ambazo bado huduma za Mahakama zinapatikana kupitia Wilaya za jirani imo kwenye mpango wa Mahakama zitakazojengwa katika Bajeti ya Mwaka 2023/24 ambapo maandalizi ya michoro ya Mahakama hiyo yamekamilika na zabuni imetangazwa ili kupata Mkandarasi wa ujenzi.

Amezitaja Mahakama zingine ambazo zimo kwenye mpango wa bajeti ya mwaka 2023/24 kuwa ni pamoja na Mahakama ya Wilaya ya Kishapu na Tarime.

Akijibu swali la nyongeza kutoka kwa Mhe. Asha Abdallah Juma aliyeteka kujua mpango wa Serikali wa kuwa na kitengo ama hotline kushughulikia malalamiko ya Wananchi wanaopata shida na usumbufu kufuatilia kesi zao  Dkt. Chana amesema tayari Mahakama ina namba maalum 0752 500 400 ambayo mwananchi anaweza kupiga kupata taarifa za kesi yake pamoja na malalamiko mengine.