Serikali Yaongeza Kasi Utendaji wa Mahakama Kuondoa Mrundikano wa Mashauri

Katika kuongeza kasi kwa Utendaji wa Mahakama nchini na kupunguza mrundikano wa mashauri mahakamani, Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa mwaka 2024/25, imeongeza idadi ya watendaji mbalimbali wa Mahakama ikiwemo Majaji kumi na Mahakimu 91, hivyo kufikisha Jumla ya Majaji 146 na Mahakimu 1,426.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro leo Jumatano Aprili 30, 2025 Bungeni Jijini Dodoma wakati akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara yake kwa mwaka 2025/26 akieleza kuwa kupunguza mrundikano wa mashauri mahakamani ni moja ya vipaumbele muhimu vya Serikali katika kuhakikisha kuwa wananchi wanapata haki kwa wakati.
"Katika kipindi cha Julai Mwaka 2024 hadi Aprili Mwaka 2025 kulikuwa na jumla ya mashauri takribani 238,154 mahakamani, kati ya hayo mashauri 63, 050 yalikuwepo mwanzoni mwa Julai 2024 na mashauri 175,104 yalifunguliwa." Ameeleza Waziri Damas Ndumbaro.
Waziri Ndumbaro pia ameeleza kuwa kati ya mashauri 238,154 yaliyokuwepo, mashauri 174,581 yalisikilizwa na kuhitimishwa na mashauri 63,573 yanaendelea katika hatua mbalimbali huku mashauri yenye umri mrefu mahakamani yakiwa ni 2,780 sawa na asilimia 4 ya mashauri yote yaliyobakia kwenye Mahakama mbalimbali za nchini Tanzania.
"Kati ya mashauri yenye muda mrefu yaliyopo mahakamani, mashauri 1,325 yapo Mahakama ya Rufani, 189 yapo Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya rushwa na uhujumu uchumi. Jumla ya mashauri 59 yalibakia mwishoni mwa Juni 2024, 118 yalisajiliwa, 108 yalisikilizwa na 69 yalibakia."
Waziri Ndumbaro pia ameeleza kuwa katika kipindi cha Julai 2024 hadi Aprili 2025 Serikali imeendelea na ujenzi na ukarabati wa majengo ya Mahakama ambapo Serikali inaendelea na ukarabati wa Jengo la Mahakama kuu Dodoma na Iringa, Ujenzi wa vituo jumuishi vya utoaji haki kwenye mikoa 9 pamoja na maendeleo ya ujenzi wa Mahakama za Wilaya 11 na mahakama za mwanzo 72 katika mikoa mbalimbali.