Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

TANZANIA YAWEKA WAZI  MSIMAMO WAKE KUHUSU MAPENZI YA JINSIA MOJA KATIKA  BARAZA LA UN

Imewekwa: 16 Nov, 2026
TANZANIA YAWEKA WAZI  MSIMAMO WAKE KUHUSU MAPENZI YA JINSIA MOJA KATIKA  BARAZA LA UN

Tanzania imesisitiza kutounga mkono mapendekezo yanayotaka kuhalalisha mapenzi ya jinsia moja na kuondoa adhabu kwa makosa ya kujamiiana kinyume na maumbile, ikieleza kuwa msimamo huo unazingatia sheria za nchi, mila, desturi, tamaduni na maadili ya jamii ya Kitanzania.

Msimamo huo umesomwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Hamis Ulega (Mb), wakati wa kuwasilisha msimamo wa Tanzania kuhusu mapendekezo yaliyotolewa katika mchakato wa Mapitio ya Hali ya Haki za Binadamu kwa Nchi (UPR) unaofanyika chini ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.

Katika kueleza msimamo huo, Serikali imebainisha kuwa Tanzania haijaunga mkono mapendekezo yanayotaka kuhalalishwa kwa mahusiano ya jinsia moja, yakiwemo yanayotaka kuondolewa kwa adhabu kwa makosa ya kujamiiana kinyume na maumbile. Serikali imesisitiza kuendelea kuzingatia sheria zilizopo pamoja na mila, desturi, tamaduni na maadili ya jamii ya Kitanzania.

Aidha, Tanzania imeeleza kuwa haijaunga mkono jumla ya mapendekezo 68 kwa sababu mbalimbali, zikiwemo kutofautiana kwa baadhi yake na misimamo ya kitaifa kuhusu masuala mahsusi, pamoja na hitaji la kufanya utafiti, tathmini na mashauriano zaidi kuhusu athari zake za kisheria, kisera, kijamii na kiuchumi.

Serikali imefafanua kuwa maamuzi kuhusu kuridhia mikataba ya kimataifa na kufanya mabadiliko ya sheria yanayogusa maisha ya wananchi yanahitaji kufuata taratibu za kikatiba na kuhusisha mamlaka husika, ikiwemo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hata hivyo, Tanzania imekubali mapendekezo yanayohimiza kuchunguza uwezekano wa kuridhia mikataba hiyo ili kutoa nafasi kwa tathmini na mashauriano kabla ya maamuzi ya mwisho.

Msimamo huo unaonesha namna Tanzania inavyoshughulikia masuala ya haki za binadamu kwa kuzingatia wajibu wake wa kimataifa, sheria za nchi na mazingira ya kijamii, huku ikisisitiza umuhimu wa kufuata taratibu za kikatiba katika maamuzi yanayohusu mustakabali wa wananchi.