TANZANIA, ICC ZAAHIDI KUIMARISHA USHIRIKIANO NA KUBADILISHANA UZOEFU
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Athuman Katimba (Mb.), amekutana na Rais wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), Mhe. Jaji Tomoko Akane, na kuwasilisha msimamo wa Tanzania kuhusu ushirikiano na Mahakama hiyo. Mazungumzo hayo yamefanyika leo Novemba 13, 2026 pembezoni mwa Mkutano wa Kimataifa wa Upatikanaji wa Haki unaoendelea Sun City, Afrika Kusini.
Mhe. Katimba amesema Tanzania, kama nchi mwanachama wa Mkataba wa Roma, inaendelea kutekeleza kwa dhati misingi na malengo ya mkataba huo na mfumo mpana wa haki jinai wa kimataifa. Amesema amani endelevu, haki na uwajibikaji ni misingi muhimu ya demokrasia, utawala bora na heshima ya utu wa binadamu.
Mhe Katimba amebainisha maeneo ya kipaumbele kwa ushirikiano na ICC ikiwemo, kubadilishana uzoefu wa mageuzi ya kisheria, ushirikiano wa kimahakama, ulinzi wa wahanga na mashahidi, mafunzo kwa majaji na waendesha mashtaka, na elimu kwa umma kuhusu Mkataba wa Roma.
Kwa upande wake, Jaji Akane ameipongeza Tanzania kwa hatua inazochukua kuimarisha haki, na kusema ICC ipo tayari kuendelea kushirikiana nayo. Amesema kwamba Ofisi ya Msajili wa Mahakama hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine inaweza kusaidia kuwezesha utoaji wa mafunzo na kuzijengea uwezo mahakama za Tanzania.
Mhe. Katimba amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na ICC kwa kuzingatia kanuni za ukamilishano (complementarity), mamlaka ya kitaifa, uhuru wa mahakama na utawala wa sheria.