Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Wananchi Tumieni Kikamilifu Fursa Mbalimbali Zinazobuniwa na Serikali – Dkt. Chana

Imewekwa: 04 Oct, 2023
Wananchi Tumieni Kikamilifu Fursa Mbalimbali Zinazobuniwa na Serikali – Dkt. Chana

Na William Mabusi – WKS

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ametoa wito kwa wananchi kutumia kikamilifu fursa mbalimbali zinazobuniwa na Serikali na ambazo zinaigharimu Serikali fedha nyingi.

Balozi Dkt. Chana ametoa wito huo wakati akihutubia mamia ya wananchi waliofurika kwenye uwanja wa Mwanga Community Centre wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Usajili wa Watoto wa Umri Chini ya Miaka Mitano Mkoani Kigoma, tarehe 03 Oktoba, 2023.

Mpango huo ambao unasogeza huduma ya usajili karibu na maeneo ya makazi yaani katika Ofisi za Watendaji Kata na katika Vituo vya Tiba unatekelezwa na Serikali kupitia Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali wa Maendeleo wenye lengo la kutambua haki za watoto, kuboresha hali ya usajili wa vizazi nchini kwa kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma kwa maendeleo ya Taifa.

Pamoja na usajili wa watoto Dkt. Chana akatoa wito kwa watu wazima kusajili na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa, “na sasa RITA imerahisisha upatikanaji wa huduma kwani waweza kutuma maombi ya huduma kidijitali  popote ulipo kwa kutumia mfumo wa eRITA. Serikali inawekeza fedha nyingi kubuni mipango hivyo wananchi tutumieni fursa hizo kikamilifu.”

Mpango huo umezinduliwa nchini mwezi Juni mwaka 2013 na hadi sasa zaidi wa watoto 8,646,324 wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa kwenye mikoa 24 ambayo mpango huu umetekelezwa. Katika kutekeleza mpango huo mkoani Kigoma jumla ya watoto 396,182 wanatarajiwa kusajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa. Mhe. Chana akatoa wito kwa kaya zenye watoto walio chini ya miaka mitano kushiriki kikamilifu kwenye zoezi hilo.