WATALAAM WA SHERIA WAAJIRIWE KUANZIA NGAZI ZA KATA

Wadau mbalimbali wanaotoa huduma za Kisheria Wilayani Kasulu Mkoa wa Kigoma wametoa wito kwa serikali kuajiri wataalamu wa sheria kuanzia ngazi za kata ili kusogeza huduma karibu zaidi kwa wananchi.
Wadau hao ambao ni mashirika na taasisi zinazohusika na utoaji wa huduma za kisheria, wametoa wito huo leo Septemba 23, 2025 walipotembelewa na Bodi ya kitaifa ya Msaada wa Kisheria.
Wamesema huduma zikisogezwa ngazi za kata wananchi watafikiwa na kupata msaada wa kisheria kwa uharaka huku wakiomba serikali iwezeshe kuboreshwa kwa miundombinu ya kufanyia kazi ikiwemo upatikanaji wa ofisi kwa mashirika yanayotoa huduma za msaada wa kisheria.
Kwa upande wao wajumbe wa bodi ya msaada wa kisheria wametoa wito kwa mashirika yanayotoa msaada wa kisheria kujua mipaka ya majukumu yao wawapo mahakamani, kwa kuepuka kufanya kazi za uwakili na badala yake kujikita katika kutoa ushauri wa kisheria.
Ziara ya bodi ya msaada wa kisheria Wilayani Kasulu imelenga kukusanya maoni ya wadau kuhusu maboresho ya Sera ya Msaada wa Sheria, hususan katika maeneo yanayohitaji kuimarishwa ili kuhakikisha usimamizi na utoaji wa huduma za kisheria unafanyika kwa ufanisi.