WATUMISHI NA WANANCHI ZAIDI YA200 WAPATA HUDUMA ZA MSAADA WA KISHERIA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA

Jumla ya Watumishi na wananchi 231 waliotembelea Banda la Wizara ya Katiba na Sheria wakati wa Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma wamepatiwa huduma za msaada wa Kisheria pamoja na Elimu ya Haki, Uraia, Utawala Bora pamoja na Utatuzi wa migogoro.
Hayo yamebainishwa leo Juni 23, 2025 na Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Abdulrahman Msham, wakati wa zoezi la ungaji Rasmi wa maadhimisho hayo yaliyoanza Juni 16, 2025 katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.
Msham alisema kuwa wananchi wengi waliofika katika Banda la Wizara walikua na changamoto zilizohitaji Elimu, Ushauri pamoja na Ufumbuzi.
Aidha Msham, alibainisha kuwa migogoro ya Ardhi imekuwa mingi ikifuatiwa na migogoro ya mirathi pamoja na ndoa.
"Katika idadi ya watu tuliowahudumia, wenye Migogoro ya Ardhi walikua wengi, wakifuatiwa na mirathi na ndoa, na hata katika kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia iliyotekelezwa Nchi nzima, takwimu ya migogoro ya Ardhi ni kubwa ikifuatiwa na mirathi na ndoa" alisema.
Aliongeza kuwa " Mirathi Ina kuwa na takwimu kubwa kwa kuwa warithi wengi wanakuwa wakigombania Ardhi " .
Msham alisema kuwa kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia pamoja na maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma, Wizara imechukulia changamoto za wananchi kama fursa na kwa kushirikiana na Wizara na Taasisi nyingine za kisekta iko tayari kuweka mkazo katika changamoto hizo ili kuzitatua na kumaliza migogoro yote kwa Nia ya kuwa na Tanzania salama yenye wananchi wanaofaham Katiba na Sheria na kufuata Sheria kwa manufaa ya Nchi.
Aliongeza pia Wizara ya Katiba na Sheria itashiriki maonyesho ya 49 ya bishara ya kimataifa yatakayofanyika katika viwanja vya sabasaba Temeke jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 28 Juni 2025 ambapo itaendelea kutoa huduma za msaada wa Kisheria pamoja na Elimu ya Haki Uraia na Utawala Bora.