Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

WAZIRI NDUMBARO AKAZIA: WIZARA YA KATIBA NA SHERIA NI NGOME YA UTAWALA NA USIMAMIZI WA HAKI

Imewekwa: 21 Jul, 2025
WAZIRI NDUMBARO AKAZIA: WIZARA YA KATIBA NA SHERIA NI NGOME YA UTAWALA NA USIMAMIZI WA HAKI

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, amewataka wakurugenzi na menejimenti ya wizara hiyo kuongeza ubunifu na kuibua fursa zitakazosaidia wananchi kutatua changamoto zao.

Waziri Ndumbaro alisisitiza kuwa Wizara ya Katiba na Sheria ni wizara ya utawala na usimamizi wa haki, akihimiza umuhimu wa kuhakikisha majukumu yanatekelezwa kwa wakati na kwa weledi.

Alisema hayo Julai 18, 2025 katika Kikao Kazi kinachofanyika katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere, Kibaha, Pwani, ambacho kinalenga kutathmini utendaji wa wizara kwa mwaka wa fedha 2024/2025 na kuweka mikakati mipya ya kuongeza ufanisi kwa mwaka 2025/2026.

Akifafanua zaidi, Waziri Ndumbaro alibainisha kuwa kutokana na uwepo wa Dira ya Taifa 2050, wizara haina budi kuanza kuweka mikakati ya kutekeleza mipango yake kwa kuihusianisha na maono na misingi mikuu iliyobainishwa katika dira hiyo. Alitaja misingi hiyo kuwa ni pamoja na:Kusimamia misingi ya Utawala Bora,Amani, Usalama na Utulivu kwa Kuheshimu Katiba, Demokrasia, Sheria na Haki za Msingi

Awali, Katibu Mkuu wa wizara Ndg. Eliakim Maswi alisema kuwa kikao kazi hiki    kitajumuisha  uwasilishwaji  wa mada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukumbushana majukumu ya kiongozi bora,utendaji kazi na  usimamizi wa rasilimali za Serikali.

Kikao kazi hiki muhimu kinajumuisha timu ya viongozi wa wizara, wakurugenzi wa idara, na vitengo na kinatarajiwa kuweka msingi imara wa utekelezaji bora wa majukumu ya wizara katika kipindi kijacho.