Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

WIZARA YAHITIMISHA SABASABA KWA KUHUDUMIA WANANCHI 4133; YAPATA ZAWADI NA TUZO

Imewekwa: 13 Jul, 2025
WIZARA YAHITIMISHA SABASABA KWA KUHUDUMIA WANANCHI 4133; YAPATA ZAWADI NA TUZO

Wizara ya Katiba na Sheria imehitimisha rasmi leo Julai 13,.2025 ushiriki katika maonesho ya 49 ya Biashara ya kimataifa (Sabasaba) kwa kutoa huduma mbalimbali za kisheria kwa Wananchi 4133 jijini Dar Es Salaam wanaume wakiwa 1925 huku wanawake wakiwa 2213.

Mkurugenzi Msaidizi wa Haki za Binadamu Beatrice Mpembo amesema Wizara imeanza kushiriki maonesho hayo kuanzia tarehe 26 Juni, 2025 hadi leo Julai 13, 2025 na wananchi waliotembelea banda la wizara hiyo wamepewa uelewa wa masuala mbalimbali yanayo yetekelezwa npamoja na huduma za masaada wa kisheria.

“Tumeweza kutoa elimu kwa wananchi hasa kwa wao kujua haki zao, masuala ya katiba, elimu kuhusu masuala ya ardhi, ndoa, mirathi, kesi za jinai na madai, kiukweli tumeweza kutoa huduma bora ambayo imewezesha Wizara ya Katiba na Sheria kuwa Mshindi wa Kwanza kati ya Wizara zote zilizoshiriki maonesho haya”, ameeleza Mpembo.

Ameongeza kuwa maonesho haya yanapoisha huduma za msaada wa kisheria zinaendelea kutolewa katika ofisi za halmashauri za wilaya zote ambapo kuna madawati ya msaada wa kisheria hivyo wananchi wenye matatizo waende kwenye halmashauri zote za Mkoa wa Dar es Salaam watahudumiwa.

Aidha Mpembo ameongeza kuwa Wizara ya Katiba na Sheria imepata zawadi kutoka kwa Mkurugenzi wa Winifrida Flower iliyotoa huduma ya mapambo na usafi katika banda hilo ambaye ameipongeza wizara kwa ushindi na kwa kutoa huduma bora huku akiwashukuru kwa ushirikiano alioupata.