Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Dkt. Ndumbaro Azindua Kanuni za Watoa Taarifa

Imewekwa: 02 Mar, 2023
Dkt. Ndumbaro Azindua Kanuni za   Watoa Taarifa

Na Mwandishi wetu, Dodoma

Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt Damas Ndumbaro amezindua Kanuni za Watoa Taarifa na Ulinzi wa Mashahidi za mwaka 2023 na kueleza kuwa Kanuni hizo zitasaidia kufichua uhalifu na kuimarisha utoaji haki jinai.

Dkt Ndumbaro ameyasema hayo wakati wa kuzindua Kanuni hizo hatua ambayo inaashiria kuanza utekelezaji wa Sheria ya Watoa Taaarifa na Ulinzi wa Mashahidi ya mwaka 2016.

Katika uzinduzi huo ambao umefanyika tarehe 28 Februari, 2023 Dkt. Ndumbaro amesema kanuni hizo zinaenda kusaidia uimarishaji utoaji wa haki jinai kwa sababu zinahusu utoaji wa taarifa za ukiukwaji wa sheria mbalimbali, makosa ya jinai, wizi wa mali za umma na ufisadi.

“Watoa taarifa hizi ni muhimu sana kwenye jamii, wanatwambia mali ya umma inaibiwa. Katika historia ya nchi hii watoa taarifa wamesaidia kufukua mambo mengi yenye maslahi kwa jamii lakini walikuwa hawatambuliki kisheria.”

Aidha, Dkt Ndumbaro alisema sehemu ya pili ya kanuni hizo ni ulinzi wa mashahidi na kuwa ni eneo ambalo lilikuwa limelegalega hasa kwenye mfumo wa haki jinai.

“Kuna wakati mashahidi walikuwa wanaogopa kwenda kutoa ushahidi wakihofia madhara ya wao kutoa ushahidi.” Dkt Ndumbaro alisema uwepo wa sheria na kanuni hizo zinabeba mambo makuu matatu ambayo ni utawala bora, utoaji wa haki jinai na zinakoleza vita ya mapambano dhidi ya uhalifu.

“Tunaamini uzinduaji wa kanuni hizi unaenda kuwa chachu ya watu kuibua makosa mengi zaidi yanayofanyika kwa sababu wanakinga kisheria na kikanuni.”

 Vilevile, Dk Ndumbaro ameagiza kufanyika kwa mafunzo na utoaji elimu kwa watanzania na kusisitiza kuwa sheria hiyo ikitumika vizuri mali za umma zitaokolewa.

“Wale wadokozi wadokozi, arobaini zao zimefika kwani sheria na kanuni hizi, zinakwenda kulinda uchumi wa nchi na kuwaumbua na kuwaanika wahalifu na kwenda kupunguza uhalifu unao waathiri sana wananchi.”

Pia Dkt. Ndumbaro amezitaka mamlaka zinazopaswa kupokea taarifa hizo za uhalifu kuhakikisha  zinafika  kwenye vyombo vya dola ambavyo navyo vinatakiwa kutekeleza kwa haraka, hatua itakayoongeza imani kwa watoa taarifa.

Dkt. Ndumbaro alisema pia kanuni hizo zitavisaidia vyombo vya habari ambavyo navyo vimekuwa vikipokea taarifa kutoka kwa watoa taarifa na hapo nyuma ulinzi ulikuwa ni maadili na sasa vitakuwa na kinga ya kisheria.

Naye Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Khatib Kazungu alisema watoa taarifa na mashahidi ni watu muhimu katika mnyororo wa haki jinai kwani taarifa wanazozitoa zinawezesha kufichua uhalifu kwenye jamii, na mashahidi wamekuwa wakiongeza ufanisi katika uendeshaji wa mashauri ya jinai kwa wakati.

 “Uwepo wa kanuni hizi utawezesha wananchi kujisikia huru, kutoa taarifa zozote za uhalifu uliofanyika au unaopangwa kufanyika na pia utawafanya mashahidi kuwa huru kutoa ushahidi mahakamani kwani zinawahakikishia ulinzi hatua ambayo itasaidia kuongeza imani.”

Awali, Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Ufuatiliaji Haki, Bw. Kharist Luanda alisema kanuni hizo zinaweka mfumo wa kisheria wa kuwatambua, kuwalinda, kuwalipa fidia na kuwapatia zawadi watoa taarifa na mashahidi kulingana na taratibu na vigezo vilivyowekwa kwenye kanuni.