Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Huduma ya Msaada wa Kisheria Kufika Hadi Vijijini

Imewekwa: 16 Feb, 2023
Huduma ya Msaada wa Kisheria Kufika Hadi Vijijini

Na Farida Khalfan - WKS

Serikali za Tanzania Bara na Zanzibar Kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo wameungana kutekeleza kampeni ya Kitaifa ya Huduma ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inayotekelezwa kwa miaka mitatu kuanzia Februari 2023 hadi Februari 2026.

Kampeni hii itaangalia zaidi upatikanaji haki kwa watu wasiojiweza hususan wanawake na watoto, haya yakiwa ni maagizo ya Rais kuwa kupata haki ni haki ya mwananchi.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro ameyasema hayo wakati akizindua kampeni hiyo Leo Februari 15, 2023 katika hoteli ya Four Points jijini Dar es Salaam.

Dkt. Ndumbaro amesema Serikali za Tanzania Bara na Zanzibar na Wadau wa Maendeleo kila mmoja alikuwa anatoa Huduma ya Msaada wa Kisheria kivyake lakini kuanzia sasa itafanyika kwa pamoja na kufikia ambapo hapakufikiwa mikoa yote Tanzania Bara na Zanzibar.

Dkt. Ndumbaro amesisitiza kuwa "Huu ni mkakati ambao lazima tutekeleze kwa nguvu zote na utagusa maeneo kama kutoa elimu ya haki za Binadamu, kupambana na ukatili wa kijinsia, Masuala ya mirathi, migogoro ya ardhi na mifumo ya Sheria".

Vilevile, Dkt. Ndumbaro amesema Wasaidizi wa Kisheria 4790 kutoka Tanzania Bara na 370 kutoka Tanzania Zanzibar wamepatiwa mafunzo kuhusiana na haki za Binadamu na Msaada wa Kisheria hivyo watakuwa Msaada mkubwa katika kutekeleza kampeni hii kwa ufanisi.

Aidha, Wadau wa Maendeleo wakiwemo GIZ, UNICEF, UNDP na LSF wameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali kutekeleza kampeni hii.

Pia Wadau wengine kama TLS, TAWJA, LHRC, TANLAP, CHRAGG na TAWLA wamesema wataendelea kutekeleza Huduma ya utoaji Msaada wa Kisheria ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa kampeni hii.

Naye, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Katiba, Sheria na Utawala Bora Zanzibar Bi. Mansura Kassim amesema kila mdau achukue nafasi yake ili kuona kiini cha uvunjwaji wa haki ikiwemo unyanyasaji kwani vitendo hivyo  vimekuwa vikiongezeka badala ya kupungua japokuwa adhabu kali zimekuwa zikitolewa.

Aidha, akifunga hafla hiyo Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Geophrey Pinda amesema jamii inatakiwa iwe wazi na kuzungumza kwa kila kiashiria cha ukiukwaji wa haki ili hatua za haraka za kuzuia zichukuliwe.

Mhe. Pinda ameongeza kuwa kila mwaka kutakuwa na tathmini ya kupima kampeni inavyotekelezwa ili kuona kama Kuna matokeo tarajiwa.

Sheria ya Msaada wa Kisheria ilianza kutekelezwa mwaka 2017 baada ya kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.