Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Kamati ya Bunge Yaridhishwa na Majibu ya Serikali

Imewekwa: 24 Jan, 2024
Kamati ya Bunge Yaridhishwa na Majibu ya Serikali

Na William Mabusi - WKS Dodoma

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Florent Kyombo imeridhishwa na majibu ya hoja zote kumi zilizowasilishwa na Bunge kwa Wizara ya Katiba na Sheria mwezi Februari, 2023.

Kikao cha Kamati hiyo kimefanyika tarehe 23 Januari, 2024 kwenye kumbi za Bunge ambapo Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akiongozana na Katibu Mkuu wa Wizara Bi. Mary Makondo, baadhi ya Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara na Wataalamu alitoa majibu ya hoja hizo.

Hoja zilizowasilishwa na Bunge ni pamoja na Miswada inayosomwa Bungeni kwa lugha ya Kiswahili itafsiriwe kwa lugha ya Kiingereza ili kuwasaidia watumiaji wasiojua lugha ya Kiswahili, Serikali iharakishe mchakato wa kusanifu programu ya kutafsiri mwenendo wa mashauri na hukumu za Mahakama kutoka katika Lugha ya Kiingereza kwenda katika Lugha ya Kiswahili ili kurahisisha upatikanaji wa haki kwa haraka, Serikali kutilia mkazo elimu kwa wadau na wananchi kuhusu umuhimu na faida za utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala, miongoni mwa zingine.

Akisoma majibu ya hoja hizo kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, Mkurugenzi wa Sera na Mipango Bw. Mbaraka Stambuli amesema tangu kufanyika kwa mabadiliko ya Tafsiri ya Sheria Sura ya 1, Kiswahili kilifanywa kuwa lugha ya kutungia sheria. Katika kujibu hoja ya Bunge, kifungu hicho kimefanyiwa tena marekebisho kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali Na. 3 ya mwaka 2023 ili kuitaka Serikali kuhakikisha kuwa Sheria yoyote inayotungwa kwa lugha ya Kiswahili inatafsiriwa kwenda Lugha ya Kiingereza ndani ya siku 90 baada ya kuanza kutumika.

Bw. Stambuli ameendelea kusema kuwa ili kurahisisha zoezi la kutafsiri hukumu na kumbukumbu za kimahakama kwa lugha ya Kiswahili, Mahakama imeanza kutumia Mfumo wa Kunukuu na Kutafsiri Kumbukumbu za Kimahakama (Translation and Transcription System – TTS), hatua itakayoongeza kasi ya maamuzi na mienendo ya kimahakama kupatikana kwa lugha ya Kiswahili.

Aidha, Serikali inaendelea na uhakiki wa Sheria 258 zilizotafsiriwa katika lugha ya Kiswahili ili zitangazwe katika Gazeti la Serikali na kuanza kutumika. Pia, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imepanga kutafsiri sheria kuu 188 zilizobakia.

Katika kuongeza ufanisi wa utekekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ili  kuharakisha kukamilika kwa kesi za jinai, kufanikisha zoezi la kutenganisha shughuli za mashataka na upelelezi, Serikali imeandaa Mpango Kabambe wa miaka mitano (2023/2024 - 2027/2028) ambao unahusisha ujenzi wa majengo ya ofisi, upatikanaji wa vitendea kazi, ununuzi wa vifaa vya TEHAMA na magari.

Katika kufanikisha zoezi la utenganishaji wa shughuli za upelelezi na mshtaka Ofisi mpya za wilaya 50 zimefunguliwa na hivyo kufanya kuwa na jumla ya Ofisi 92 za Wilaya na kubakiwa na wilaya 47 ambazo hazina Ofisi.

Akijibu hoja ya utoaji wa elimu kwa wadau na wananchi kuhusu umuhimu na faida za utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala. Amesema Wizara kwa kushirikiana na Taasisi zilizo chini ya Wizara imekuwa ikitumia matukio ya kitaifa kama vile Wiki ya Sheria, Wiki ya Msaada wa Kisheria, Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, Maonesho ya Wakulima ya Kitaifa na Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa kila mwaka kutoa elimu ya sheria pamoja na utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala kwa umma na wadau wengine.

Aidha, Wizara ya Katiba na Sheria imefanya marekebisho ya Sheria ya Usuluhishi Sura ya 15 ya mwaka 2020 kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Sekta ya Sheria ya mwaka 2023 kwa madhumuni ya kuimarisha mfumo wa usuluhishi wa migogoro kwa njia mbadala nchini.

Akihitimisha majibu ya hoja hizo Dkt. Chana amesema Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Taasisi zilizo chini ya Wizara itaendelea kutekeleza maoni na mapendekezo ya Kamati kadri inavyoelekezwa kwa maslahi mapana ya nchi.