Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Shinyanga bado yaandamwa na ukatili wa kijinsia

Imewekwa: 15 Jun, 2023
Shinyanga bado yaandamwa na ukatili wa kijinsia

Na Lusajo Mwakabuku – WKS Shinyanga

Mkoa wa Shinyanga umetajwa kuendelea kukabiliwa na matukio ya ukatili wa kijinsia ikiwemo vipigo, mimba na mauaji na sababu kuu ikitajwa kuwa ni jamii kuendelea kushikilia mila na desturi zilizopitwa na wakati, elimu ndogo pamoja na jamii kutokuwa tayari kutoa taarifa ya matukio hayo.

Afisa Ustawi wa Jamii wa Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga ambaye ni mmoja wa wataalam wanaoetekeleza Mama Samia Legal Aid Campaign (MSLAC) mkoani humo, bwana Leopold Hamza aliyasema hayo wakati akitoa elimu ya kijinsia wakati timu hiyo ya wataalam ilipokutana na wananchi wa vijiji vya Mwamagunguli na Galamba vya kata ya Kolandoto mkoani Shinyanga ambapo mada mbalimbali za kisheria pamoja na msaada wa kisheria vilitolewa kwa wananchi hao tarehe 14/06/2023.

Afisa Ustawi wa Jamii huyo alisema bado changamoto za ukatili ni tatizo ikiwemo ukatili wa utumikishwaji wa watoto katika shughuli mbalimbali zikiwemo katika mashamba ya tumbaku, migodi midogo na majumbani, masuala ya ubakaji na ulawiti, mimba za utotoni zinazokatisha ndoto za watoto pasipo kujali sheria ya mtoto ya mwaka 2009 na ile ya ajira.

“Kinachosikitisha zaidi ni kwamba jamii inawafahamu wakosaji na mara nyingine kuwalinda kwa kuamua kumalizia kesi nyumbani au kutotoa taarifa mapema wanapoona vitendo vya ukatili. Hali hii hutoa mwanya kwa watuhumiwa kurudia vitendo hivyo mpaka siku inayopelekea kifo.  Hii inarudisha nyuma maendeleo ya nchi na juhudi za Serikali katika kuleta maendeleo na kufikia usawa wa kijinsia na maendeleo endelevu” Alisema bwana Leopold.

“Ndugu zangu wa Kolandoto tupaze sauti unapofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia au kuona mtu akifanya vitendo hivyo basi chukua hatua kwa kuripoti tukio katika madawati ya Polisi ya kijinsia vilevile unaweza kutoa taarifa ya tukio katika ofisi za Ustawi wa Jamii, Serikali za Mitaa, Vituo vya afya, Vituo vya msaada wa kisheria ili kupata huduma kwa wakati, msaidie mwathirika kuripoti tukio lake ndipo tunaweza kutokomeza vitendo hivi.” Aliongeza bwana Leopold.

Naye mratibu wa timu hiyo ya wataalam kutoka Wizara ya Katiba na Sheria bwana George Mollel ambaye ni Wakili wa Serikali alitoa mada kuhusu haki za Watoto. Alieleza kuwa mtoto ni mtu yeyote mwenye umri chini ya miaka kumi na nane na haki za mtoto zinajumuisha haki ya kushirikiana na wazazi wote wawili, kutambuliwa kibinadamu na kupatiwa mahitaji ya msingi ya ulinzi wa mwili, chakula, elimu, huduma ya afya, huku akifafanua sheria zinazofaa kwa ukuaji wa mtoto, haki za kiraia za mtoto, uhuru wa kutokubaguliwa kutokana na jinsia, ulemavu, dini, kabila au sifa nyingine. 

Wakili Mollel aliongeza kuwa ulinzi na usalama wa mtoto sio jukumu la Maafisa wa ustawi wa jamii peke yao bali ni jukumu la Taifa kwa ujumla na kwamba hakuna anayeruhusiwa kumdhuru, kumuumiza au kumnyonya mtoto. Yeyote anayejua kwamba kuna mtoto anayeonewa au kutendewa vibaya hana budi kutoa taarifa kuhusu vitendo hivyo kwa; Ustawi wa jamii, Polisi - Dawati la jinsia na Watoto, ofisi za Serikali za Mtaa, Taasisi na Mashirika ya kijamii pamoja na kupiga simu namba 116 ya kitaifa isiyo na  tozo kwa lengo la kumlinda mtoto.

Aidha bwana Mollea aliwasisitiza wale wote ambao wana changamoto binafsi na wamekosa nafasi au hawako huru kueleza changamoto zao katika mikutano hiyo, kufika katika mabanda yanayotoa huduma za kisheria mjini Shinyanga ambapo wataalam wapo hapo wakitoa huduma hadi tarehe 21 Juni mwaka huu.

Wakitoa salaamu za kuhitimisha mikutano hiyo kwa nyakati tofauti Wenyeviti wa vijiji hivyo vya Mwamagunguli na Galamba vya Kata ya Kolandoto walimshukuru Mhe. Rais kwa kuwaletea kampeni hii huku wakieleza kuwa katika vijiji vyao, ukatili wa kijinsia licha ya kwamba bado upo lakini umepungua baada ya wananchi kuelimishwa kupitia mikutano ya vijiji, ikiwemo wanandoa kutelekeza familia na wanafunzi kuachishwa shule. Na hili limetokana na mikakati iliyowekwa na Serikali katika kutoa elimu pamoja na kuwaonesha wananchi ni wapi pa kupeleka malalamiko na kesi zao zinazohusu ukatili wa kijinsia katika jamii, kazi ambayo Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inaendelea kuifanya hivi sasa.

Mama Samia Legal Aid Kampeni inayoongozwa na kauli mbiu inayosema ”Msaada wa kisheria kwa haki, usawa, amani na maendeleo” imedhamiria kuongeza wigo wa ufikiwaji haki kwa wananchi, hususan walio vijijini na  ambao hawawezi kumudu gharama za Mawakili. Kampeni hii pia imekuwa msingi mzuri wa kujenga uelewa wa wananchi kuhusu haki zao za kikatiba na kisheria; jambo ambalo ni muhimu katika kulinda na kukuza haki za binadamu nchini. Hii ni kampeni ya miaka mitatu yenye lengo la kufikia mikoa yote nchini huku ikitarajiwa kuhitimishwa mwaka 2026.