Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Suala la Miradi ya Serikali Kutozwa Kodi Kufikishwa Bungeni

Imewekwa: 12 Mar, 2024
Suala la Miradi ya Serikali Kutozwa Kodi Kufikishwa Bungeni

Na Lusajo Mwakabuku – WKS IRINGA

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Joseph Mhagama amesema ni wakati sasa Serikali kuangalia kama kuna tija katika kutoza miradi ambayo inatengenezwa kwa ajili ya wananchi kwani kufanya hivyo si kwamba kunaongeza mlolongo wa utekelezaji wa miradi hiyo peke yake bali pia kunaongeza gharama katika kupitia hatua za upatikanaji wa msamaha wa kodi katika miradi ya Serikali.

Mhe. Mhagama ameyaongea hayo baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa Mahakama katika Mikoa ya Iringa, Njombe na Ruvuma tarehe 12 Machi, 2024 ikiwa ni sehemu ya ziara ya Kamati hiyo katika kukagua miradi ya maendeleo kwa taasisi zilizo chini ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria.

Mhe. Mhagama alisema kuwa kwake anaona suala hilo halina tija na ni ajenda watakayoenda nayo bungeni kwani tayari hiyo miradi inaandaliwa kwa lengo la kumsaidia mwananchi hivyo hata makusanyo ya kodi hizo ni kwamba mapato yake yanarudi katika kumhudumia mwananchi hivyo ni bora badala ya fedha hizo kurudi hazina zitumike katika kuharakisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

“Kwanza ngoja niwaambie kupatikana kwa msamaha wa kodi ni process, ina mlolongo wake mrefu ambao umesababisha baadhi ya miradi kutoendelea kwa zaidi ya mwaka kusubiria mchakato huo kukamilika. Hela zenyewe zote ni za Serikali ni sawa na  kutoa fedha mkono wa kulia kuhamishia mkono wa kushoto. Mbaya zaidi tunachelewasha huduma kwa wananchi wakati wa kufuatilia msamaha hii ya kodi.” Alisema Mhe. Mhagama.

Awali akimkaribisha Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Joseph Mhagama na kamati yake, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana alisema anamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha miradi mbalimbali ndani ya Wizara ya Katiba na Sheria inayolenga kusogeza karibu miundombinu ya utoaji haki kwa wananchi ikiwemo miradi ya ujenzi wa mahakama mbalimbali nchini huku akibainisha kwamba suala hili limeendelea kuongeza imani kwa wananchi kuhusu mahakama ikiwemo matumizi ya teknolojia katika usajili na uendeshaji kesi unaorahisisha kesi nyingi kusikilizwa ndani ya muda mfupi.

Mhe. Chana alisema “kama moja ya jitihada za kupunguza kero kwenye baadhi ya maeneo yenye watu na migogoro mingi mahakama ilikuja na wazo la Mahakama inyotembea yaani Mobile Court. Kwa jitahada hizo, tumefanikiwa kupunguza mrundikano wa Mashauri hadi kufikia 4%.”

Waziri Chana pia akaongeza “Tume ya Kuboresha Haki Jinai imependekeza namna tunavyoweza kuboresha upatikanaji haki kwa masuala ya Jinai ambayo Wizara yetu imeyachukua na inayafanyia kazi ikiwemo matumizi ya TEHAMA kwa upande wa Mahakama kwa mfano mfumo wa mashauri ufahamikao kama Advance Case Management System ambao umeunganishwa na mifumo kadhaa ya wadau, mfumo wa kutafsiri na kutunza kumbukumbu na pia kusikiliza mashauri kwa njia ya Video yaani Video Conference Board.”

Mtendaji Mkuu wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mahakama alisema “kufanikiwa kwa Mahakama kunatokana na uongozi mzuri wa Jaji Mkuu ambaye ana maono makubwa, lakini pia ushrikiano mkubwa wa mihimili mitatu ndio unaopelekea utekelezaji wa majukumu yetu kuwa rahisi katika kutoa huduma.”

“Hadi hivi sasa tumefanikiwa kujenga Mahakama za mwanzo 960 na lengo likiwa ni kufikia Mahakama 3000 nchini kote. Hivi sasa tuna wilaya 139 lakini mahakama zipo 135 zimebakia mahakama 4 tu katika kuhakikisha kila wilaya ina Mahakama nchini.  Aidha, katika Ukanda wa Kusini na Mashariki mwa Afrika, Mahakama ya Tanzania ndio inaongoza katika matumizi ya TEHAMA katika utoaji haki kwa wananchi. Hivi sasa Hakimu anaweza maliza kesi halafu akapata nakala ya kesi ya kurasa 200 chini ya dakika mbili kwa Kiswahili kupitia mfumo wa AI” Alisema Ole Gabriel.

Katika utekelezaji wa miradi hiyo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama aliongeza kuwa katika viwango vya ubora wa usimamizi wa miradi ya Mahakama vilivyowekwa na Benki ya Dunia katika miradi yake, Tanzania imefikia asilimia 89 ya ubora wa utekelezaji wa miradi, kiwango ambacho ni cha juu zaidi duniani katika miradi ya Mahakama inayotekelezwa na Benki ya Dunia.

Akielezea changamoto za Wakandarasi katika miradi hiyo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama alisema kuna baadhi ya Wakandarasi ambao walipewa kazi nao wakawapa kazi watu wengine na mbaya zaidi wakawa hawana taarifa yeyote juu ya uendelezwaji wa miradi husika suala lililopelekea Mtendaji wa Mahakama kugoma kulipa mpaka suala hilo liwekwe sawa.

Akihitimisha ziara hiyo mkoani Iringa, Mhe. Mhagama alisifia utendaji wa Mahakama na kwamba wao kama kamati ya taasisi hizi wanatembea kifua mbele kutokana na ubunifu,  na utekelezaji wa miradi aidha akaiagiza Mahakama kuangalia namna ya kugawanya masurufu katika utekelezaji miradi kwa kuanzia na Tarafa, Majimbo na hatimaye Kata katika kujenga Mahakama.

“Tutashirikiana na Wizara kuhakikisha kuwa bajeti ya Mahakama inakidhi mahitaji kwani ndio muhimili pekee wenye kazi kubwa katika kuhakikisha utulivu na amani inapatikana nchini”. Alisema Mhe. Mhagama.