MAFUNZO YA SHERIA KWA WANAHABARI KUCHECHEMUA MAPAMBANO DHIDI YA UKATILI WA KIJINSIA TARIME
Wizara ya Katiba na Sheria inaendesha mafunzo maalumu kwa waandishi wa habari kutoka katika Wilaya ya Tarime mkoani Mara kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kuripoti kwa usahihi masuala ya kisheria, haki za binadamu na matukio ya ukatili wa kijinsia yanayoathiri jamii.
Akifungua mafunzo hayo Wilayani Tarime, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, amesema mafunzo hayo yataongeza tija katika utoaji wa habari za kisheria na kusaidia wananchi kutambua haki zao kupitia vyombo vya habari.
Amesema katika kipindi cha hivi karibuni kumekuwa na matukio mbalimbali ya ukatili wa kijinsia yanayoripotiwa katika vyombo vya sheria, hali inayohitaji ushiriki wa wanahabari katika kutoa elimu na taarifa sahihi kwa wananchi.
"Endapo mtatumia mafunzo haya kwa ufasaha, yataongeza tija katika kuhabarisha wananchi kuhusu mafanikio ya huduma za msaada wa kisheria pamoja na changamoto zinazojitokeza katika jamii zetu," amesema Gowele.
Kwa upande wake Mratibu wa mafunzo hayo kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Wakili wa Serikali Athumani Msosole amesema mafunzo hayo yatawawezesha wanahabari kutambua namna bora ya kuripoti masuala yanayohusu ukiukwaji wa haki za binadamu, changamoto za kisheria pamoja na hatua zinazochukuliwa katika kutatua matatizo hayo ndani ya jamii.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari Tarime, Jacob Karoli, amesema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka kwani wanahabari wengi wanahitaji maarifa zaidi ya masuala ya kisheria yatakayowasaidia kuandika habari zenye usahihi na manufaa kwa jamii.
Jumla ya wanahabari 40 wa Tarime wanashiriki mafunzo hayo yanayotarajiwa kuwawezesha kuwa mabalozi wa elimu ya sheria, haki za binadamu na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia katika maeneo yao