RAIS MWINYI ASISITIZA LENGO LA SERIKALI LA KUENDELEA KUIMARISHA MIFUMO YA SHERIA
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi amesisitiza kuwa serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya sheria Nchini ikiwemo kutunga sera ya huduma ya Msaada wa Kisheria Nchini ili kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa na mifumo ya Haki nchini Tanzania.
Rais Mwinyi amesema hayo leo Jumamosi Juni 20, 2026 katika Viwanja vya Dole, Kizimbani Visiwani Zanzibar wakati akizindua awamu ya pili ya msaada wa Kisheria ya Mama Samia, akisema serikali imefikia hatua hiyo ili kuhakikisha kila mwananchi hasa wanyonge wanafikiwa na huduma za kisheria kwa haraka na ufanisi.
"Haki ya mwanadamu katika Jamii yoyote hususani inayozingatia utawala wa sheria ni msingi wa utawala wa bora. Tangu kuasisiwa kwa Taifa letu jambo la msingi na la kipaumbele ni kuhakikisha haki inapatikana kwa wote na kwa usawa na ili kufikia malengo hayo serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya kisera na kisheria yenye kusimamia upatikanaji wa haki." Amesema Rais Mwinyi.
Rais Mwinyi amebainisha hatua ambazo zinatekelezwa na serikali kuwa ni pamoja na kampeni hiyo ya msaada wa kisheria pamoja na uanzishwaji wa madawati ya Msaada wa kisheria katika Halmashauri zote 184 za Tanzania bara ili kurahisisha utoaji wa haki Nchini pamoja na kuanzisha huduma kwa Mteja, programu yenye kupokea na kushughulikia malalamiko, changamoto na migogoro ya kisheria kote Nchini.
"Serikali pia imeunda mfumo wa kidigitali wa kuhakikisha uzingatiaji wa matakwa ya kisheria kwa watoa huduma za msaada wa kisheria, kupokea na kuchambua data za msaada wa kisheria na kuwezesha rufaa kutoka sehemu moja kwenda nyingine pamoja na kuwezesha wananchi kupata mssada wa kisheria na mrejesho wa haraka juu ya masuala yao waliyowasilisha, lengo ni kuwezesha huduma kiganjani kwa kila mwananchi mwenye simujanja na wasiokuwa na simujanja." Amesema Rais Mwinyi.
Katika hatua nyingine Rais Mwinyi pia amewapongeza Mawaziri wa Sheria kutoka pande zote za Muungano, wadau na wataalamu walioshiriki kwenye awamu ya kwanza ya Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia, akisema kampeni hiyo imekuwa chachu kubwa katika kuhakikisha wananchi hususan wasiokuwa na uwezo wanaifikia haki kwa wakati na kwa ufanisi.