Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

TUTAENDELEA KUSOGEZA HUDUMA ZA MSAADA WA KISHERIA KARIBU NA WANANCHI- RAIS MWINYI

Imewekwa: 22 Jun, 2026
TUTAENDELEA KUSOGEZA HUDUMA ZA MSAADA WA KISHERIA KARIBU NA WANANCHI- RAIS MWINYI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi amesema kuzinduliwa kwa awamu ya Pili ya Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ni hatua muhimu yenye kulenga kuendelea kusogeza huduma za kisheria kwa wananchi wa Tanzania.

Aidha licha ya hatua hiyo, Rais Mwinyi wakati akihutubia wananchi katika uzinduzi wa Kampeni hiyo kwa awamu ya pili leo Jumamosi Juni 20, 2026 katika viwanja vya Dole, Kizimbani Visiwani Zanzibar, amesema serikali pia imeendelea kuchukua hatua za makusudi za kuimarisha huduma za msaada wa kisheria, kwa kutunga sera itakayotoa muongozo wa usimamizi na uendeshaji wa huduma za msaada wa kisheria.

"Hatua hii italeta mabadiliko makubwa ya kimtazamo na kimfumo katika utoaji wa huduma za msaada wa kisheria. Katika hilo serikali imedhamiria kutumia fursa za TEHAMA zilizopo Nchini kusanifu na kujenga mifumo ya kielektroniki zitakazorahisisha utoaji wa huduma za msaada wa kisheria." Amesema Dkt. Mwinyi.

Rais Mwinyi ameendelea kusema kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha misingi ya uwazi na uwajibikaji katika kutoa huduma za msaada wa kisheria na kurahisisha ukusanyaji, utunzaji na uchakataji wa takwimu.

Rais Mwinyi amesema ni dhamira ya serikali kuondoa kabisa vikwazo vinavyosababisha wananchi kutofikia haki, kwa kuweka mifumo ambayo itawafikia wananchi wote Nchini hususani Vijana pamoja na makundi maalumu.