Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Bunge laridhia Muswada wa Marekebisho ya Sheria

Imewekwa: 01 Nov, 2023
Bunge laridhia Muswada wa Marekebisho ya Sheria

Na William Mabusi – WKS Dodoma

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesoma kwa mara ya tatu Bungeni Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali za Sekta ya Sheria wa mwaka 2023 (The Legal Sector Laws (Miscellaneous Amendments) Bill, 2023) na kuridhiwa na Bunge na sasa utapelekwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo naye akiridhia Muswada huo utakuwa sheria.

Muswada huo unaolenga kufanyia marekebisho sheria Ishirini na Tatu ili kuondoa upungufu uliobainika wakati wa utekelezaji wa Sheria hizo umesomwa tarehe 31 Oktoba, 2023 Bungeni Jijini Dodoma.

Kati ya Sheria Ishirini na Tatu zinazotegemea kurekebishwa ni Sheria ya Ushahidi, Sura ya 6 ambapo kifungu cha 127 kinapendekezwa kurekebishwa ili kuwezesha ushahidi wa mtoto wa umri mdogo kupokelewa bila kujali kuwa mtoto alitoa ahadi ya kuwa atasema kweli na kwamba hatasema uongo. Lengo la marekebisho haya ni kuondoa changamoto ya tafsiri mahakamani ambapo ushahidi wa mtoto umekuwa haupewi uzito endapo mtoto hakutoa ahadi ya kuwa atasema kweli na kwamba hatasema uongo. Hali hii imesababisha watuhumiwa katika kesi nyingi hususan kesi za ukatili kwa watoto kuachiwa huru kutokana na kukosekana kwa uthibitisho wa ahadi ya mtoto. Madhumuni ya marekebisho haya ni kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto kwa kuruhusu ushahidi wa watoto hao kupokelewa mahakamani bila kufungwa na masharti ya kiufundi.

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria Mhe. Yahaya Massare Mbunge wa Manyoni Magharibi kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati amesema Serikali imezingatia kwa kiasi kikubwa maoni ya Kamati na kuliomba Bunge kupokea Muswada huo, kuujadili na kuupitisha.